Na Mwandishi Wetu, Lindi na Mtwara
Katika jitihada za kuongeza uelewa wa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na Rufaa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi ya Umma (NeST), Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa mafunzo kwa wazabuni, wajasiriamali na watumishi wa Umma waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Akielezea kuhusu mafunzo hayo ya siku tano (kuanzia tarehe 16 - 20 Februari, 2026), Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Sheria (PPAA), Bi. Florida Mapunda amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa Umma kuhusu taratibu za uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Ununuzi wa Umma. “Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka sharti la lazima kwa ununuzi wa umma kufanyika katika mfumo wa NeST. Kutokana na sharti hilo, PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuwasaidia wadau wa ununuzi wa umma (Wazabuni na Taasisi za Umma) kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki,” amesema Bi. Mapunda.
Pamoja na mambo mengine, Bi. Mapunda ameongeza kuwa Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST ina manufaa makubwa kwa wazabuni kwani inarahisisha uwasilishaji wa malalamiko ya zabuni kwa njia ya mtandao bila kufika ofisini, jambo linalochangia kuokoa muda, gharama na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ununuzi wa Umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Rufaa kutoka PPAA, Bi. Violet Limilabo ameeleza kuwa PPAA ina mchango mkubwa katika kulinda haki za wazabuni kwa kuwapa fursa ya kusikilizwa wanapoona hawakutendewa haki katika michakato ya Ununuzi wa Umma.
Aidha, PPAA imeendelea kuimarisha uwazi na usawa kwa kuhakikisha taratibu za ununuzi wa umma zinafuatwa kwa mujibu wa sheria na kupunguza migogoro kwa kutoa suluhisho la kisheria.
Naye Afisa Ununuzi kutoka ofisi za PPRA Kanda ya Kusini, Bw. Aziz Njovu alitoa mafunzo kuhusu moduli mpya za majadiliano (negotiations) na uandaaji, upekuzi na utiaji saini wa Mkataba (Contract preparation, vetting and signing kwenye mfumo wa NeST, alisema kwa sasa mchakato wa majadiliano na utiaji saini wa mkataba unahitimishwa kwa njia ya mtandao.
“Matumizi ya mfumo wa NeST yameendelea kuimarisha uwajibikaji na kurahisisha ufuatiliaji wa mikataba ya ununuzio wa umma,” amesema Bw. Njovu.
Mafunzo hayo yamewahusisha jumla ya washiriki 322 ambao ni wataalamu wa sheria, Tehama na ununuzi pamoja na wazabuni, makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalum pamoja na mafundi wa ndani.
Mafunzo kuhusu Matumizi ya Moduli ya kupokea na Kushughulikia Malalamiko na Rufaa katika Mfumo wa NeST yaligawanyika katika makundi matatu ambapo Kundi la kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (tarehe 16 Februari, 2026), Mkoa wa Lindi (tarehe 17 na 18 Februari, 2026) na Mkoa wa Mtwara (tarehe 19 na 20 Februari, 2026)
.jpeg)

.jpeg)


Post A Comment: