Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara jijini Mwanza,ili  kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ushindani wa soko pamoja na taratibu za kupata haki katika shughuli za kibiashara yaliyoandaliwa na Baraza la Ushindani wa Soko (FCT).

Na.Mwandishi Wetu-MWANZA

 BARAZA  la Ushindani wa Soko (FCT)  limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara jijini Mwanza, yakilenga kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ushindani wa soko pamoja na taratibu za kupata haki katika shughuli za kibiashara.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, ambapo waliipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa juhudi zake za kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji kupitia uwepo wa chombo huru cha kusimamia na kudhibiti ushindani wa soko.

Akifungua semina hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana, alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wadau wa sekta ya biashara kwani yanawawezesha kuelewa kwa kina majukumu ya Baraza la Ushindani pamoja na umuhimu wa mshikamano katika utekelezaji wa sheria za ushindani.

“Kupitia semina hii, wadau watapata uelewa mpana kuhusu Baraza la Ushindani na nafasi yake katika kulinda haki za mlaji pamoja na kuendeleza ushindani wa haki katika soko.”Alisema Bw.Elikana

Akizungumza katika mafunzo hayo, Msajili wa Baraza la Ushindani, Bw. Mbegu Kaskasi, alisema kuwa Baraza lipo kwa ajili ya kulinda masuala yote yanayohusu ushindani wa soko na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini. Alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Baraza unalenga kuimarisha misingi ya utawala bora kwa kuhakikisha sheria za ushindani zinatekelezwa kikamilifu, kwa haki na kwa uwazi.

Aidha, aliongeza kuwa Baraza huhakikisha mamlaka za udhibiti zinazingatia taratibu na kanuni za ushindani wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kutoa majibu sahihi na ya haraka katika migogoro ya kibiashara. Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kumlinda mlaji dhidi ya vitendo vinavyodhoofisha ushindani, hivyo kuchangia katika ujenzi wa uchumi shindani, jumuishi na wenye tija kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Chemba ya Wafanyabiashara, Bw. Hassan Karambi, alisema kuwa amepata elimu yenye manufaa makubwa kupitia programu ya Baraza ya kuwajengea uwezo wadau.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia wafanyabiashara kufahamu kuwa endapo hawataridhika na maamuzi ya mamlaka za udhibiti kama LATRA, TCRA, TCAA, EWURA, PURA pamoja na Tume ya Ushindani (FCC), wana haki ya kukata rufaa katika Baraza la Ushindani ili kupata haki yao.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa, Bi. Imelda Salumu, alifafanua utaratibu wa Baraza katika kupokea rufaa kutoka kwa wadau.

Alisema kuwa malalamiko huanza kwa mtoa huduma husika, na endapo hayatapatiwa ufumbuzi, hufikishwa katika mamlaka ya udhibiti kama hatua ya kwanza ya rufaa. Aliongeza kuwa iwapo mlalamikaji hataridhishwa na maamuzi ya mamlaka hiyo, utaratibu humruhusu kuwasilisha rufaa katika Baraza la Ushindani kwa hatua zaidi za kisheria.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Alex Sonna

Post A Comment: