Ndani ya kipindi kifupi cha siku 100 za uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sekta ya Madini imeendelea kujiimarisha kama moja ya vielelezo bora vya mageuzi ya kiuchumi yanayoongozwa na maono, Sera thabiti na utekelezaji wenye mwelekeo wa kimataifa. Sekta ya Madini imepiga hatua kubwa si tu katika ukusanyaji wa mapato, bali pia katika uongezaji thamani wa madini, ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) maendeleo ya teknolojia na nafasi ya Tanzania katika ramani ya madini duniani.

Ukuaji wa Mapato na Mchango kwenye Uchumi wa Taifa

Takwimu zinaonesha mabadiliko Chanya na ya msingi, ndani ya miezi mitatu pekee (Novemba 2025 hadi Januari 25, 2026), Sekta ya Madini imekusanya kiasi cha Shilingi bilioni 311, sawa na asilimia 103 ya lengo ndani ya kipindi hicho, mwenendo huo unaakisi mageuzi ya mifumo ya usimamizi, udhibiti na uwazi katika shughuli za madini. Kwa ujumla, mapato ya Serikali kutoka sekta hiyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 526 Mwaka wa Fedha wa 2020/2021 hadi zaidi ya shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025, huku mwaka wa fedha uliopo wa 2025/2026 sekta ikiwekewa lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.2.

Mafanikio haya yamechochea mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa (GDP) kuongezeka kutoka asilimia 10.1 hadi asilimia 12 ndani ya siku 100 pekee. Hatua hii inaipa Tanzania nafasi ya kipekee miongoni mwa nchi za Afrika zinazotumia rasilimali zao za madini kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi jumuishi.

Local Content: Watanzania Kuwekwa Kwenye Moyo wa Sekta

Moja ya mafanikio makubwa yenye athari chanya ya kijamii na kiuchumi ni utekelezaji wa Sera na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), kupitia marekebisho ya Kanuni za mwaka 2018, Serikali imeweka mfumo unaohakikisha ajira, manunuzi na huduma migodini zinawanufaisha Watanzania moja kwa moja. Matokeo yake, ajira za Watanzania migodini zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia zaidi ya 18,800 mwaka 2024, sawa na zaidi ya asilimia 97 ya ajira zote migodini.

Kwa upande wa manunuzi, mageuzi haya yamepunguza utegemezi wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi ambapo manunuzi ya ndani yameongezeka hadi asilimia 88 ya manunuzi yote ya migodini kufikia mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 62 mwaka 2018. Hatua hiyo imesaidia kubakiza mzunguko mkubwa wa fedha ndani ya nchi na uchumi wa Taifa, kukuza viwanda vya ndani na kuongeza ajira katika sekta shirikishi kama ujenzi, usafirishaji, nishati na huduma za kitaalamu.

Uongezaji Thamani na Viwanda: Kuondoka kwenye Uchimbaji wa Malighafi

Katika utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009, Serikali imeongeza kasi ya ujenzi wa viwanda vya kusafisha na kuongeza thamani ya madini ambako Mkoa wa Dodoma umeibuka kama kitovu kipya cha uongezaji thamani, ukiwa na viwanda 9 vya uongezaji thamani wa madini pamoja na viwanda 4 vya madini ya metali kama shaba na nikeli. Aidha, kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kiwanda cha kusafisha chumvi kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara kimekamilika kwa asilimia 99, hatua inayoongeza thamani ya rasilimali kabla ya kuingia sokoni.

Uwezeshaji wa Wachimbaji Wadogo: Mageuzi ya Uchumi wa Wananchi

Wachimbaji wadogo, wanaohusisha zaidi ya Watanzania milioni 6 kwenye mnyororo wa thamani wa madini, wamekuwa kitovu cha mageuzi ya kijamii. Ndani ya siku 100, Serikali imenunua mitambo 15 ya uchorongaji miamba, kutoa leseni 511 kwa vikundi vya wachimbaji wadogo Geita na Shinyanga, na kuwezesha mkopo wa Shilingi bilioni 30 kupitia taasisi za fedha. Sambamba na hilo, mpango wa kununua mitambo mikubwa ya CIP yenye uwezo wa kuchenjua tani 120 kwa saa, pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa dhamana, umefungua ukurasa mpya wa uchimbaji wa kisasa, salama na wenye tija.

Miradi Mikubwa na Hadhi ya Kimataifa

Katika hatua ya kihistoria, Tanzania inajiandaa kuingia rasmi kwenye uzalishaji wa Madini ya Ferro-Niobium kupitia mradi wa Songwe, Panda Hill, Mbeya, unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 1. Mradi huo utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa kimataifa wa madini haya muhimu kwa viwanda vya chuma na teknolojia ya juu. Sambamba na hilo, maandalizi ya utafiti wa kina wa dhahabu (High Resolution Airborne Geo-Physical Survey) na kampuni ya kimataifa ya Barrick Gold katika Nzega na Kahama yanaashiria uwekezaji mpya wa kiwango kikubwa mara baada ya Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kuzindua urushwaji wa helkopta kwa ajili wa utafiti huo.

Dhahabu, Nishati Safi na Masoko ya Ndani

Kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ununuzi wa zaidi ya tani 17 za dhahabu umeiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 bora barani Afrika kwa hifadhi ya dhahabu, jambo linaloongeza uthabiti wa uchumi na heshima ya kifedha kimataifa. Wakati huohuo, uzalishaji wa nishati safi ya kupikia ya ‘Rafiki Briquettes’ unaotokana na makaa ya mawe kupitia STAMICO unaunga mkono ajenda ya nishati safi, ukipunguza utegemezi wa kuni na mkaa ili kulinda mazingira.

Hitimisho

Kwa mtazamo wa kimkakati, siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia zimeifanya Sekta ya Madini kuwa chombo cha mageuzi ya uchumi, ajira na hadhi ya Taifa kimataifa. Tanzania inaendelea kujizatiti na kujiimarisha kuelekea kwenye uchumi wa uongezaji thamani, teknolojia na ushiriki mpana wa wananchi. Hayo si mafanikio ya kawaida, bali ni mapinduzi ya kimuundo yenye athari chanya za kudumu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.














Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: