Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali inachukua hatua katika kuimarisha uwezeshaji wanawake kiuchumi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu mifuko ya maendeleo inayowanufaisha wanawake.

Akizungumza Mei 6, 2026 bungeni jijini Dodoma, Mhe. Mahundi amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata taarifa na kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), ikiwa ni pamoja na kushirikiana na taasisi za fedha na wadau wa maendeleo kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara kupitia makongamano ya kikanda.

 “Serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, TAMISEMI pamoja na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuhakikisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yanapatiwa mafunzo na fursa za mikopo nafuu.” amesema Mhe. Mahundi

Katika swali lingine, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifuko iliyopo badala ya kuanzisha mipya, ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali. 

"Kupitia ushirikiano na Benki ya Dunia, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza utoaji wa mikopo kupitia mradi wa PAMOJA, hatua itakayopanua wigo wa wanawake kunufaika na fursa za kiuchumi". amesema Mhe. Mahundi

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Share To:

Post A Comment: