Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea ugeni wa viongozi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu Duniani (IAEA) ukiongozwa na Bwana Gashaw Gebeyehu Wolde, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika, pamoja na Bi. Azza Kashlan, Afisa wa Usimamizi wa Programu.

Ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na IAEA katika sekta za viwanda, afya, elimu, kilimo na chakula.

Ugeni huo, ukiwa na mwenyeji wake Profesa Najat Kassim Mohammed, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), ulianza ziara yake jijini Dodoma kwa kutembelea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambapo walikutana na Katibu Mkuu, Mhe. Balozi Dkt. Samweli William Shelukindo.

Mazungumzo hayo yalihusu nafasi ya Tanzania katika ushirikiano wa kimataifa wa nyuklia kwa maendeleo endelevu.


Baadaye, viongozi hao walitembelea Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu, Profesa Daniel Mushi, kuhusu mafanikio ya miradi inayotumia teknolojia ya nyuklia nchini.


Aidha, walijadili maendeleo ya programu za elimu zilizoanzishwa kwa msaada wa IAEA, ambazo zinalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa fizikia ya tiba ili kuimarisha huduma za saratani nchini.


Naibu Katibu Mkuu alibainisha kuwa ushirikiano wa Tanzania na IAEA ni wa muda mrefu na umeleta matokeo ya vitendo kupitia Programu ya Ushirikiano wa Kiufundi. Kikao hicho kilikumbusha mafanikio ya hivi karibuni, yakiwemo miradi ya kitaifa ya TC inayoendelea katika awamu ya mwaka 2025–2026 na kiwango cha juu cha maendeleo kilichoripotiwa kufikia mwisho wa Desemba 2025.


Miradi hiyo inahusu sekta za viwanda, afya, kilimo na usalama wa chakula, ikiwemo; Mradi wa kituo cha mionzi cha matumizi mbalimbali (multipurpose irradiator facility), Upanuzi wa huduma za tiba ya nyuklia na radiotherapy, Uzalishaji wa mbegu kwa njia ya mionzi (mutation breeding) kwa pamba na maharage ya kawaida, Kuimarisha uwezo wa maabara ya usalama wa chakula Zanzibar.


Katika kikao hicho, Profesa Mushi aliwasilisha mapendekezo kwa awamu ijayo ya ushirikiano, ikiwemo; Kusaidia Tanzania katika matumizi ya teknolojia za nyuklia na atomu kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa usambazaji wa umeme, Kuimarisha na kusasisha mitaala ya shule na elimu ya juu katika sayansi ya nyuklia na fani zinazohusiana, Kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya maabara na uwezo wa kiufundi, Kupanua vyanzo vya nishati ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa taifa, Kuendelea kutoa mwongozo wa kiufundi kwa matumizi salama na yenye uwajibikaji ya teknolojia ya nyuklia.




Naibu Katibu Mkuu alisisitiza Kuimarisha ushirikiano kwenye mifumo na miundombinu, hususan katika: Uchambuzi wa uwezekano wa utekelezaji wa Mitambo Midogo ya Nyuklia (Small Modular Reactors – SMRs), Kupanua huduma za tiba ya mionzi ya saratani (radiotherapy) kwenda katika mikoa mingine, Matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika chakula na kilimo, na Usalama na ulinzi, ikijumuisha uboreshaji wa miundombinu ya usimamizi wa taka za mionzi (radioactive waste management facilities).




Naye Mkurugenzi Gashaw kutoka Wakala wa Nguvu za Atomu Duniani alipongeza mapendekezo hayo na kuthibitisha kuendelea kwa ushirikiano. Walisisitiza kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na shirika hilo, na sasa imefikia hatua ya ukomavu katika programu zake, huku ikichukua nafasi ya kuwa kitovu cha kikanda katika kujenga uwezo wa kitaalamu.


Mambo muhimu yaliyosisitizwa ni pamoja na; Kuendelea kuunga mkono vipaumbele vya kitaifa kupitia Programu ya Ushirikiano wa Kiufundi, Hatua za awali katika mchakato wa kuanzisha mradi wa nyuklia, ikiwemo kuimarisha taasisi, mifumo na rasilimali watu, Kutambua uongozi wa Tanzania na mchango wake katika kujenga uwezo wa kikanda, Kuendeleza matumizi ya kituo cha mionzi cha matumizi mbalimbali, Kupanua matumizi ya nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa, Kuweka usalama na ulinzi kama msingi wa matumizi ya nyuklia, Kuendeleza rasilimali watu kupitia mafunzo ya muda mrefu katika tiba ya nyuklia na fani nyingine maalumu, huku wakihimiza wataalamu wa Kitanzania kuchangamkia nafasi zinazotolewa na IAEA.




Ugeni huo pia ulitembelea Wizara ya Nishati, ambapo ulipokelewa na Katibu Mkuu Mhandisi Felichism Mramba. Mazungumzo yalihusu hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Tanzania kuelekea kuanzisha mradi wa umeme wa nyuklia, hatua inayolenga kuongeza vyanzo vya nishati safi na salama kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.


Mnamo tarehe 4 Februari 2026, ugeni huo utatembelea Chuo cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia Afrika (NM-AIST) Jijini Arusha, ambapo watajionea maendeleo ya mradi wa Green House for Beans (RAF5059). Mradi huo unatumia mbinu za nyuklia kuboresha uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde, ukilenga kuongeza usalama wa chakula na kipato kwa wakulima wadogo.


Ziara ya viongozi wa IAEA nchini Tanzania inaendelea kuthibitisha dhamira ya serikali ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika matumizi salama na endelevu ya teknolojia ya nyuklia. Kupitia miradi hii, Tanzania inalenga kuimarisha huduma za afya, kuongeza rasilimali watu wenye ujuzi wa kisayansi, kukuza kilimo, na kuandaa mazingira ya kuanzisha nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa.







Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: