Na OWM-TAMISEMI, Dodoma

Serikali imezitaka Halmashauri zote nchini kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo inayoanza Julai 2026, ikiwemo Dira ya Taifa ya 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31).

Akifungua Kikao Kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Fedha na Uhasibu kilichofanyika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma leo Februari 19, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. Sospeter Mtwale, amesema mafanikio ya mipango ya Serikali yanategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kukusanya na kusimamia mapato yao ipasavyo.

“Kama Serikali haitakusanya mapato ya kutosha, hatutaweza kuwapatia wananchi huduma bora wala kufikia malengo ya kitaifa tuliyojiwekea,” amesema.

Kikao hicho cha siku mbili kitajadili hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na maandalizi ya makadirio ya mwaka 2026/27.

Bw. Mtwale amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato si suala la hiari bali ni wajibu wa kimfumo unaohitaji nidhamu, uwazi na uwajibikaji.

 Amesema bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho, hasa katika upangaji wa malengo ya ukusanyaji, usimamizi wa vyanzo vipya vya mapato na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.

“Ni lazima tuandae makadirio ya mapato kwa uhalisia, tukizingatia uwezo wa kiuchumi wa maeneo yetu na fursa zilizopo,” ameeleza.

Katika hatua ya kuimarisha ukusanyaji, Serikali imeelekeza matumizi makubwa ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa mapato.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo, matumizi sahihi ya TEHAMA yatasaidia kupunguza mianya ya upotevu wa mapato, kuongeza uwazi na kuwezesha maamuzi ya haraka ya kiutendaji kwa kuzingatia takwimu sahihi.

Ameelekeza Halmashauri zote kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo kwa kuwekeza katika mifumo ya makusanyo, kuandaa mipango na bajeti inayozingatia uhalisia wa rasilimali na vipaumbele vya Taifa, kutumia takwimu sahihi katika kupanga malengo ya ukusanyaji na kuimarisha ufuatiliaji wa mikoa na Halmashauri ili malengo yafikiwe kwa wakati.

Kwa muktadha huo, viongozi wa fedha katika ngazi za Serikali za Mitaa wametakiwa kujitathmini kwa kina kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26 na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji kwa mwaka ujao wa fedha.

“Kikao hiki kitumike kubadilishana uzoefu na kuibua mbinu bunifu zitakazosaidia kuongeza mapato ya ndani kwa manufaa ya wananchi,” amesema Bw. Mtwale.

Serikali imeweka wazi kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ni msingi wa mafanikio ya mipango ya maendeleo. Wasimamizi wa fedha wametakiwa kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika kila hatua ya ukusanyaji na matumizi ya mapato.












Share To:

Post A Comment: