Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Frank Nkinda amekabidhi Hundi ya zaidi ya Bilioni moja kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu fedha zinazotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. 

Aidha, amekabidhi pia vitendea kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambavyo ni cherehani pamoja na vifaa vya uchomeleaji.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Hundi hiyo, DC Nkinda amevitaka vikundi hivyo kuitumia mikopo hiyo vizuri ili iweze kuwakwamua kiuchumi pamoja na kuhakikisha wanarudisha mikopo hiyo kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika.

“Fedha hizi zimeletwa kwa lengo la kuwasaidia na kuwakwamua wananchi kiuchumi, fedha hizi zisiwe chanzo cha ugomvi miongoni mwenu, nendeni mkazitumie vizuri ili muweze kufikia malengo mliyojiwekea kama wanakikundi “ Amesema DC Nkinda

DC Nkinda amevitaka pia vikundi hivyo kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika Halmashauri hiyo ili pia ziweze kuwasaidia katika urejeshaji wa mikopo hiyo pamoja na kuvitaka vikundi hivyo kuhakikisha wanarudisha mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kuwasaidia na wengine wanaohitaji.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mhe. Ibrahim Six amevitaka vikundi hivyo kutumia fedha hizo vizuri ili viwe mfano kwa jamii inayowazunguka 

Bi. Rose Manumba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala amewasisitiza wanufaika hao wa Mkopo wa asilimia 10 kurejesha fedha kwa wakati kusudi waweze kukopa tena na kuweza kujikwamua zaidi.

Afisa Maendeleo ya jamii (W) Bw. Judica Sumari akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo amesema mgawanyo wa fedha hizo ambao ni kiasi cha Shilingi 464,959,101 kimeenda kwa Wanawake, Shilingi 469,959,101 kwa vijana na watu wenye ulemavu ni Shilingi 232,479,550 

Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kupitia mikopo ya Asilimia 10 imeweza kutengeneza ajira 462 ikiwa wanawake ni 296, vijana 155 na  watu wenye ulemavu 11.









Share To:

Post A Comment: