Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa kwa wananchi wa Singida kupitia ujenzi wa kituo kipya cha kurushia matangazo cha TBC katika mji wa Itigi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Manyoni, mkoani Singida, Septemba 9, 2025, Dkt. Samia amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi kuhusu changamoto ya usikivu hafifu wa TBC katika mkoa huo.
“Ndugu zangu, nilipenyezewa taarifa kwamba Singida hii kama mkoa kuna uhafifu wa kusikika kwa TBC, redio yetu ya taifa. Hivyo basi jambo hili tunalishughulikia kupitia mradi wa uboreshaji wa usikivu wa TBC unaosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano (UCSAF), na tutajenga kituo cha kurushia matangazo cha redio masafa ya FM katika mji wa Itigi ili TBC iweze kusikika vizuri,” amesema.
Amesema mradi huo utawapa wananchi fursa ya kufuatilia habari na taarifa rasmi za taifa lao kupitia chombo cha habari kinachotambulika kwa uhakika na ukweli.
“Hii kuwapa fursa wananchi kusikia taarifa za taifa lao kutoka kwenye redio yenye uhakika na ukweli,” ameongeza.
Aidha, Dkt. Samia amesisitiza kuwa Singida ni miongoni mwa mikoa itakayonufaika moja kwa moja na mradi wa reli ya kisasa (SGR), hususan wilaya ya Manyoni, ambao unatekelezwa katika awamu ya tatu.
“Singida hii hasa eneo la Manyoni litapitiwa na mradi wa SGR awamu ya tatu unaopita hapa kuelekea Tabora. Mradi huu tunategemea kwamba unakwenda kuifungua Singida na kutengeneza ajira nyingi za vijana kwa sababu kutakuwa na kituo hapa, ambacho korido ya SGR itakayopita italeta shughuli nyingi za kibiashara,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo pia utafungua fursa za uwekezaji na kukuza ajira kwa vijana wa Singida na mikoa jirani.

Post A Comment: