Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema katika miaka mitano ijayo serikali itaanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa reli ya kisasa itakayopita Mtwara, Mbamba Bay hadi Mchuchuma na Liganga mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 26, 2025, Mtwara Mjini mkoani Mtwara, Dkt. Samia amesema mradi huo utakuwa kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi kwa mikoa ya kusini na Tanzania kwa ujumla.
“Katika miaka mitano ijayo tutaanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa reli ya viwango vya kisasa kuja Mtwara, kwenda Mbamba Bay mpaka kule Mchuchuma na Liganga kule Ruvuma. Mradi huu ni imani yetu kwamba unakuja kufungua siyo tu Mtwara bali ukanda wote huu wa Kusini,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na utafungua fursa za biashara, usafirishaji wa mizigo na kuunganisha maeneo ya kimkakati yenye rasilimali nyingi za taifa.
Aidha, Dkt. Samia amegusia changamoto ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Mtwara Mjini, akibainisha kuwa hatua za kudumu zinaendelea kuchukuliwa.

Post A Comment: