Maelfu ya wananchi wa Lindi Mjini leo Alhamisi Septemba 25, 2025 wanatarajiwa kumlaki na kumsikiliza Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atafanya mikutano miwili ya kampeni katika Manispaa ya Lindi.

Katika mikutano hiyo, Dkt. Samia atazungumzia Ilani ya CCM inayolenga kushughulikia mahitaji muhimu ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwemo sekta za afya, elimu, maji, nishati na barabara.

Akiwa na kaulimbiu ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”, Dkt. Samia jana aliendesha mikutano katika wilaya za Mtama na Ruangwa, ambapo aliahidi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa upande wa Lindi Mjini, Dkt. Samia anatarajiwa kuwaeleza wananchi dhamira ya Serikali ya CCM kujenga vituo vya afya katika maeneo ya Kitumbikweta, Rutamba na Nangaru, pamoja na ujenzi wa zahanati Namkongo, Mpulwa, Mkwaya na Namtamba. Aidha, serikali imepanga kukarabati kituo cha afya Rutamba na kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Wilaya.

Katika sekta ya barabara, amepanga kusimamia ujenzi wa barabara za kiwango cha lami ikiwemo Mtange–Kinengene Kibaoni (km 5), Bohari–Ofisi za NIDA (km 1.5), Mahakama–Mitwero, na Kikwetu–Kibumbwi. Vilevile, barabara zenye mteremko mkali katika maeneo ya Muhimbili, Matopeni, Mtanda, Mwenge na Wales zitajengwa kwa kiwango cha zege.

Mbali na miradi hiyo, Dkt. Samia ameweka mkazo katika kukuza fursa za ajira kwa vijana kupitia mikopo ya halmashauri, uwezeshaji wa wanawake na wenye ulemavu, pamoja na uanzishaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na misitu katika kila wilaya nchini.

Share To:

Post A Comment: