Wajumbe wa Bodi ya SELF Microfinance wamewatembelea wajasiriamali wawili Mkoani Arusha ambao ni kati ya wanufaika wa mikopo nafuu inayotolewa na mfuko huo.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Paul Sangawe pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Santieli Yona, wamejionea namna wajasiriamali hao walivyoweza kukuza biashara zao.

Mfuko huo upo chini ya chini ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha ulianzishwa tangu 2015 na tayari watu zaidi ya 300,000 wamepata manufaa ya kukua ki-uchumi.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza, wajasiriamali hao wamesema hawajawahi kujuta kupata mkopo huo, wamepata manufaa makubwa, biashara zao zimekua kwa kasi na kuinuka ki-uchumi.

“Nimeweza kutoka kufuga kuku 400, sasa nina kuku 1,200. Awali nilikuwa naokota mayai ‘trei’ 12 kwa siku sasa hivi naokota ‘trei 30 kwa siku,” amesema Teddy Mtinangi.

Ameieleza bodi hiyo kwamba awali alikuwa anapata faida TZS 900,000 hadi TZS 1 Mil. lakini baada ya kupata mkopo huo anapata faida TZS 3Mil na soko likichangamka hupata hadi TZS 4 Mil.

Naye, Teddy  Mchome mmiliki wa ‘Teddyjoo naturals’ ambao wanatengeneza bidhaa za nywele na ngozi kwa malighafi ya mimea asili amesema SELF Microfinance imempa fursa ya kuongeza mtaji wake.

“Bidhaa zetu hazina viambata sumu, kabla [mkopo] tulianza na wateja wachache kwa sababu tulikuwa hatujapanuka, mtaji ulikuwa mdogo lakini tulikutana na SELF Microfinance walitusaidia,” amesema.

Amesema baada ya mtaji kukua, wameongeza uzalishaji wanauza mikoa mingi ndani na nchi pia wanao wateja sasa hadi nje ya nchi.

“Tumeajiri vijana wengi zaidi ya 30 na miongoni mwao wapo walio na ulemavu wa kusikia, wametusaidia kuelimisha jamii kuhusu bidhaa zetu.

“Tuna saluni tatu hapa Arusha tunahudumia pia tuna mawakala maeneo mengi watu waliopata bidhaa zetu wamepata matokeo mazuri,” amesema.

Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa SELF wamesema wajasiriamali hao ni mfano mzuri wa kuigwa ndani ya jamii huku pia wakitoa rai kwa wengine kuchangamkia fursa ya mikopo nafuu wanayoitoa.

Mwenyekiti wa Bodi, Paul Sangawe amewapongeza wajasiriamali hao kwa kuzingatia matumizi ya mikopo yao kwa ufasaha na uaminifu walionao katika kufanya marejesho kama walivyopangiwa.

Amesema wajasiriamali hao wawili ni kati ya watu zaidi ya 300,000 walionufaika kwa mikopo nafuu inayotolewa na Mfuko huo, tangu ulipoanzishwa mwaka 2015.

Amesema pamoja na kukopesha mikopo nafuu wajasiriamali pia hutoa mikopo nafuu kwa taasisi zinazotoa mikopo midogo midogo [Microfinance] ndani ya jamii.

“Kuna taasisi 549 ambazo zimepata mikopo kutoka kwetu, kwa miaka mitano ijayo tunakusudia kufikia watu wengi zaidi,” amebainisha.

“Sasa tunaandaa mpango mkakati tutakaoutekeleza katika miaka mitano ijayo, utakaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/50,” amesema.

Amesisitiza katika mpango mkakati huo Mfuko wa SELF umedhamiria kufikia wajasiriamali wengi zaidi ili wanufaike na mikopo nafuu kukuza biashara zao na shughuli zao za ki-uchumi ili kupunguza umaskini.







Share To:

Post A Comment: