Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Viongozi Wanawake duniani (WPL), Neema Lugangira ameshauri wahariri kuhakikisha wanatumia kwa usahihi teknolojia ya Akili Unde (AI) wakati wa Uchaguzi Mkuu kuepusha madhara katika vyombo vya habari.

Akitoa mada ya 'Uchaguzi Mkuu na Matumizi ya AI'  kwenye mkutano wa kawaida wa TEF, jijini Dar es Salaam ameeleza katika uchaguzi kuwa kuna taarifa nyingi potofu hivyo AI inaweza kutumika vizuri kuhakiki usahihi wa taarifa.

"Kuna faida nyingi za kutumia AI ikiwemo kusaidia kuhakiki taarifa kwa haraka, kufuatilia kauli za uchochezi hata uchambuzi wa data," amesema.

Lugangira ameendelea kueleza kuwa licha ya AI kuwa na matumizi makubwa kwenye dunia ya sasa, pia hutumika kupotosha jamii sambamba na kuharibu heshima ya mtu ama mgombea katika jamii.

Hata hivyo amesisitiza kwamba, vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kulinda maadili katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Sambamba na hayo Lugangira alikabidhi nakala 40 kwa Jukwaa la Wahariri na 20 kwa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) za mwongozo wa Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika (AAEA) kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na Teknolojia kwenye chaguzi barani Afrika ambapo miongozo hiyo alishiriki kuiandaa wakati akiwa mjumbe wa timu ya wataalamu mwaka wa 2022/2023.






Share To:

Post A Comment: