Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Waganga Wafawidhi wa hospitali za Rufaa kuzingatia mawasiliano ya awali kabla ya kumpa mgonjwa rufaa kwenda hospitali ya Kanda kwa lengo kutoa msaada wa haraka kwa mgonjwa.

Ameyasema hayo Agosti 21, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha Kikanda cha Uboreshaji wa Huduma za Tiba kati ya Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkapa na Waganga Wakuu wa Mikoa na waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za Mikoa, kilichoambatana na ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma.

Amesema hatua hiyo itawezesha mgonjwa kusaidika kabla ya na wakati wa kusafirishwa na pia itapunguza gharama ambazo wagonjwa hulazimika kutumia katika safari na matibabu,  hatimaye kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi.

“Kabla ya kumleta mgonjwa, tuwasiliane kwanza ili tuone kama huduma husika inaweza kupatikana kwa kubadilishana ujuzi au laa mgonjwa aletwe moja kwa moja hospitali ya kanda ya Benjamin Mkapa. Hii itasaidia sana kupunguza mzigo wa kifedha kwa wagonjwa, muda ,” amesema Dkt. Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe amewataka waganga na madaktari kutoka mikoa, rufaa na waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kuhusu huduma zinazotolewa na hospitali ya Benjamin Mkapa.

“BMH imeboresha kwa kiwango kikubwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi na nyote ni mashahidi mmejionea hivyo mnaporudi kwenye vituo vyetu muwe mabalozi wa kuelezea namna mwananchi atasaidika atakapokuja kufanya uchunguzi au kufuata matibabu katika hospitali hii ya Benjamin Mkapa,” amesisitiza.

Amewataka Waganga Wafawidhi wa hospitali za rufaa kupelekea watumishi kujifunza huduma za dharura katika kituo cha mafunzo cha kanda cha huduma za dharura, hospitali ya kanda Benjamin Mkapa ili kupunguza rufaa.








Share To:

Post A Comment: