Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kusogeza huduma za jamii na miundombinu muhimu katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kwa awamu ya pili.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Agosti 30, 2025, Dkt. Samia amesema serikali inatambua changamoto zilizopo kwenye sekta ya miundombinu, afya na elimu, na kwamba hatua mbalimbali zimepangwa ili kuhakikisha wananchi wa Gairo wananufaika.
Akizungumzia sekta ya afya, Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali ya CCM inakusudia kujenga vituo vya afya vitano pamoja na zahanati 10 ndani ya wilaya ya Gairo ili kuongeza upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi.
Vilevile, ameahidi kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Gairo, kitakachowapa vijana nafasi ya kusomea ujuzi wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujiajiri na kuajiriwa.
Katika sekta ya mifugo na biashara, Dkt. Samia ametangaza mpango wa serikali kujenga machinjio manne ndani ya wilaya hiyo ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuongeza thamani ya mifugo.

Post A Comment: