Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewafikia wadau takriban 1,450 kwa utoaji wa elimu ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane jijini Dodoma na Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya mwaka huu.
Elimu hiyo imetolewa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Baraza hilo kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika banda lake la maonesho, NEMC ilielimisha kuhusu mbinu bora za kilimo hifadhi kinachozingatia mazingira, ufugaji endelevu, uvuvi salama pamoja na kulinda vyanzo vya maji.
Aidha, wananchi na wadau waliotembelea hapo walielimishwa kuhusu umuhimu wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ya kilimo ili kupunguza athari hasi kwa mazingira.
Miongoni mwa masuala yaliyopatiwa kipaumbele ni pamoja na kuwahimiza wawekezaji kusajili miradi NEMC ili kupata vyeti vya mazingira kama kigezo muhimu cha kuendesha shughuli zao kisheria na kwa kuzingatia mazingira.
Katika maonesho hayo, wataalamu wa NEMC pia walieleza athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za shughuli za binadamu kama uchomaji moto hovyo, ukataji miti na utupaji taka kwenye mifumo ya ikolojia, hali inayochangia mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa ardhi na upungufu wa rasilimali maji.
“Tunawahimiza wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira. Elimu tunayoitoa ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kiuchumi na kijamii yanayozingatia mustakabali wa mazingira yetu,” alisema Bi. Dalia Kilamlya, Afisa Mazingira NEMC
Kwa ujumla, mwitikio wa wadau mbalimbali katika kupata elimu ya mazingira kutoka NEMC umetajwa kuwa mkubwa na wenye kuleta matumaini ya mabadiliko chanya katika namna jamii inavyoshiriki kwenye kulinda na kuhifadhi mazingira.






Post A Comment: