Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Bashungwa amesema Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza kimeeleza mpango wa kuanzisha kituo cha umahiri cha utoaji wa mafunzo kwa wafungwa ili kuwapa maarifa, ujuzi na stadi za biashara zitakazowawezesha kujikimu kiuchumi pindi wanapomaliza vifungo vyao na kutoa wito wa kuhakikisha maandalizi ya kituo hicho yanafanyika.
Ameyasema hayo Agosti 6, 2025 katika hafla ya kutunuku vyeti vya ujasiriamali na stadi za biashara kwa wafungwa, iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu Arusha.
Waziri Bashungwa pia amempongeza Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka kwa namna anavyosimamia chuo, ubunifu alionao, maono ya kutafsiri mahitaji ya jamii na taaluma zinazotolewa chuoni, na mafanikio makubwa aliyoleta katika upande wa michezo. Aidha, Waziri Bashungwa ameishukuru IAA kwa ushirikiano ambao imeutoa kwa Jeshi la Magereza katika programu ya mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara yaliyotolewa kuanzia Mei 7, 2025 kwa wafungwa takribani 170 wakiwemo wanawake 41 na wanaume 129.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza CGP Jeremiah Katungu amemshukuru Prof. Sedoyeka kwa maono ya ushirikiano katika utoaji wa mafunzo hayo, akisema kuwa tangu mashirikiano na IAA kumekuwa na matokeo chanya ikiwemo mahafali hayo ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara yaliyotolewa kwa wafungwa.
Aidha, CGP Katungu amesema mafunzo yatawafanya wahitimu kuwa wema, wenye maarifa na kuwataka kutumia mafunzo kuanzisha shughuli mbalimbali za kuwaingizia kiptao watakapomaliza vifungo vyao.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka amesema mafunzo hayo yameanzishwa kwa kutumia uhalisia wa mazingira, mahitaji ya washiriki, ambayo yalihusisha vipindi vya nadharia na vitendo juu ya stadi za uanzishaji biashara kisheria, ujasiriamali, vyanzo vya mitaji, usimamizi wa fedha pamoja na utafutaji wa masoko na mazingira ya kufanyia biashara; eneo ambalo IAA ina uzoefu mkubwa kitaaluma na kiutendaji ili kuwawezesha wafungwa kupata ujuzi wa kujitegemea mara baada ya kumaliza vifungo vyao.
Aidha, Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa IAA kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini wamejipanga kupanua programu hii kwenye magereza mengine, kutoa vifaa vya kuanzisha biashara, kusaidia wahitimu kupata mitaji kupitia mamlaka za serikali za mitaa na kutoa mafunzo endelevu na msaada kwa wafungwa waliohitimu mafunzo.
Pia, Prof. Sedoyeka ametoa rai kwa wahitimu kutendea haki fursa hii ya mafunzo waliyoyapata.
Post A Comment: