Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, ametoa wito kwa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TSLB) kuendelea kuhamasisha utamaduni wa kusoma vitabu miongoni mwa wananchi wa rika na makundi mbalimbali kama sehemu ya kuendeleza elimu jumuishi.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi tarehe 22 Julai 2025, Dkt. Hussein alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mwanajamii anapata fursa sawa ya kusoma na kujifunza kupitia huduma za maktaba, akibainisha mchango wake mkubwa katika kukuza usawa wa kielimu na maendeleo ya maarifa nchini. Alihimizwa pia kusambaza utamaduni wa usomaji kwa jamii nzima, ikiwemo huduma za maktaba maalum za watoto, ambapo pia kuna vituo vya malezi vinavyowawezesha watoto kusoma na kufurahia michezo mbalimbali kwa wakati mmoja.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa TSLB kuendelea kuhifadhi kwa ufanisi nyaraka za kihistoria na kuongeza upatikanaji wa taarifa kwa watafiti na wanafunzi kupitia mifumo bora ya rejea na taarifa. Katika kukabiliana na mahitaji ya karne ya 21, Dkt. Hussein alielekeza TSLB kuimarisha huduma zake kwa kutumia teknolojia, ikiwemo kuendeleza maktaba mtandao, mifumo ya kidijitali, na huduma bunifu kama Maktaba Kiganjani, ili kuwezesha maarifa kufika kwa wananchi kwa haraka, kwa ufanisi, na kwa uwiano wa kitaifa.
Post A Comment: