Na Munir Shemweta, WANMM

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mabaraza ya Ardhi nchini ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Suzan Kihawa ameongoza kamati yake kufanya ukaguzi wa kawaida kwenye ofisi na maghala ya kampuni za udalali kuangalia utekelezaji wa shughuli za madalali wa mabaraza ya ardhi.

 

Ukaguzi huo umehusisha kamati kuangalia leseni za biashara, kitabu cha kumbukumbu za taarifa za kazi za udalali pamoja na kuangalia iwapo kampuni za udalali zinayo maghala ya kuhifadhia mali za wadaawa zilizokamatwa.

 

Ofisi zilizotembelewa na kamati hiyo leo tarehe 25 Julai 2025 jijini Dar es Salaam ni CDJ Classic Group Ltd, Fosters and Company Ltd, Igalula Auction Mart na Tambaza Auction Mart . Upande wa maghala kamati ilitembelea ghala la kampuni ya udalali la Foosters and Company Ltd lililopo Ukonga pamoja na ghala la kampuni ya Tambaza Auction Mart lililopo Sinza Dar es Salaam.

 

Kwa mujibu wa Mhe Suzan, ukaguzi uliofanyika ni wa kawaida na unalenga kusikiliza changamoto zinazowakabili madalali wa mabaraza ya ardhi sambamba na kujua kama madalali wanafuata kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao.

 

"Ziara hii ya kamati yetu pamoja na mambo mengine ni kusikiliza changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuzifanyia kazi  ili muweze kufanya kazi zenu kwa ufanisi, najua hakuna sehemu inayokosa changamoto na mambo ni mengi na pale zinapotokea changamoto tunazifanyia kazi" amesema.

 

Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yenye jukumu la kusikiliza na kuamua mashauri yanayotokana na migogoro ya umiliki wa ardhi yanahitimisha jukumu hilo kwa kuwatumia madalali wa mabaraza kutekeleza amri zinazotolewa pale mdaawa aliyeshindwa kesi anaokaidi kutii amri husika.

 

Kamati ya uteuzi na nidhamu za madalali wa Mabaraza ya Ardhi ina  wajumbe sita wanaoteuliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao ni wataalamu waandamizi wanaowakilisha wizara  na taasisi ambazo kwa namna moja ama nyingine zinahusika katika utatuzi wa migogoro ya umiliki wa ardhi.

 

Muundo wa kamati hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 28B cha sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi Sura ya 216.






Share To:

Post A Comment: