Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa serikali yake imeanza rasmi kutoa ruzuku kwa wafugaji wa Tanzania, ikianza na ruzuku ya Chanjo kwa kuku Takribani Milioni 40, Mbuzi na Kondoo Milioni 17 pamoja na hereni za utambuzi kwa mifugo aina ya Ng'ombe.

Rais Samia amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi wa Bariadi Mkoani Simiyu, mara baada ya kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya chanjo na utambuzi kwa mifugo akitoa wito kwa wafugaji nchini kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo lenye kaulimbiu isemayo "Mifugo ni utajiri, chanja na kuitambua ili kuongeza thamani."

'Sababu mojawapo ya sekta ya mifugo kuwa na mchango mdogo kwanza ni kutotambulika na kutotumika vyema kwa rasilimali ya mifugo tuliyonayo, tulikuwa tunafuga kienyeji, tunafuga kama ni mila na desturi kwamba kufuga ni kazi yetu, lakini tulikuwa tunafuga kama fahari yetu kuwa na ng'ombe wengi lakini hao ng'ombe hawakuzalishii, tuna ng'ombe tunaishi nao miaka 15, 20 lakini wenyewe hawatuzalishii kitu." amesema Rais Samia.

Rais Samia amebainisha kuwa serikali imewekeza zaidi ya shilingi Bilioni 216 kwaajili ya Kampeni hiyo, magonjwa yanayolengwa yakiwa ni Homa ya mapafu ya Ng'ombe, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo pamoja na chanjo ya Mdondo ambayo imekuwepo kwa Kuku.

Kulingana na Rais Samia, gharama za chanjo kwa kuku zote zimebebwa na serikali sambamba na hereni za utambuzi, huku chanjo nyingine serikali na wafugaji wakichangia nusu kwa nusu, lengo likiwa ni kuiwezesha nchi kwa pamoja kuwa na kanzidata ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji na thamani ya mifugo.

Akisitiza Kampeni hiyo kuwa endelevu, Rais Samia ameeleza kuwa kwasasa mauzo ya mifugo na bidhaa za mifugo nje ya nchi yameongezeja kutoka tani 692 mwaka 2021 hadi tani 14, 701 mwaka 2024, ikiwa na thamani ya Dola Milioni 61.4, akieleza kuwa matarajio yake ni kuongeza zaidi kwa mauzo hayo mara baada ya zoezi la Chanjo kukamilika kwani kutaongeza sifa ya Tanzania katika ithibati zinazokubalika kwenye soko la mifugo na bidhaa zake.

Share To:

Post A Comment: