Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano wao mkubwa pamoja na dua na maombi yao wakati wote ambao amekuwa akiwatumikia kama Rais tangu kilipotokea kifo cha Mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Samia amebainisha hayo leo Ijumaa Juni 27, 2025 Bungeni Mjini Dodoma wakati wa kuhutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni utekelezaji wa Katiba inayomtaka kufanya hivyo ili kuruhusu shughuli za Uchaguzi Mkuu kuendelea.
"Niwashukuru waajiri wangu- Watanzania, hakika wao ndiyo chachu na hamasa ya mimi kufanya yote hayo. Nawashukuru kwa sala, dua na maombi yao bila kusahau ushirikiano mkubwa wa hali na mali katika kuijenga Tanzania tunayoitaka na Taifa linalotumainiwa"Amesema Rais Samia.
Rais Samia pia amewashukuru watangulizi wake kwenye nafasi ya Urais akiwemo Dkt. Jakaya Kikwete, akieleza kuwa msaada wao wa Kimawazo na ushauri pamoja na misingi imara waliyoiweka umemsaidia Yeye binafsi pamoja na serikali anayoiongoza, akisema palipo na Wazee hakuna jambo linaloharibika.
Rais Samia pia amemtaja Spika wa Bunge la 12 Dkt. Tulia Ackson kama Kiongozi hodari na mahiri, akimpongeza kwa kazi nzuri ya Kuongoza muhimili wa Bunge pamoja na uwakilishi wake kama Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge duniani, akiwa ni Mwanamke wa kwanza kutoka Barani Afrika kuongoza Umoja huo wa Mabunge.
"Shukrani nyingi ni kwa uongozi wako shupavu, mahiri na wenye weledi mkubwa. Hakika Mhe. Spika umeliongoza vyema Bunge hili na kukamilisha Mikutano 19 katika Bunge hili la 12. Najua haikuwa kazi rahisi lakini pia ni kazi nyepesi kwako kwani penye wengi, kuna mengi na kila mmoja na kichwa chake ndani ya Bunge hili." Amebainisha Rais Samia.
Katika Hotuba yake pia amewapongeza wabunge wa Bunge la 12 kwa uwakilishi wao mzuri wa wananchi, utungaji wa sheria na kuisimamia serikali, akiwashukuru pia kwa Tuzo waliyompatia kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika maendeleo na ustawi wa Tanzania.
Post A Comment: