Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amelielekeza Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza jitihada zake za kiutendaji katika kudhibiti Matukio ya Watu kupotea, matukio ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kadhaa na mijadala kuibuka mara kadhaa kwenye Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Juni 27, 2025 Bungeni Mjini Dodoma, wakati akihutubia na kuhitimisha shughuli za bunge la 12 la Tanzania, akisisitiza pia umuhimu wa Kikosi cha Usalama barabarani kujidhatiti katika kupunguza ajali za barabarani nchini Tanzania.

"Natoa Pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuilika kwa jitihada za jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Kasi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani imeongezeka. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani, lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake." Amesema Dkt. Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza kuwa serikali yake inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na miundombinu kwa Jeshi la Polisi nchini, akibainisha kuwa Jumla ya Vituo vya Polisi 472 vimejengwa nchi nzima hadi ngazi ya Kata kwa upande wa Bara na Shehia kwa Zanzibar.

Aidha maboresho makubwa pia yametajwa kufanyika kwenye makazi ya Askari polisi, Kununua vitendea kazi ikiwemo magari na pikipiki kwaajili ya Operesheni na kazi za utawala huku pia Jumla ya askari wapya 16,000 wakiajiriwa pamoja na kupandishwa Vyeo kwa Maafisa wakaguzi na Askari 10,363.

Share To:

Post A Comment: