
TUME ya Madini imetoa leseni 8, 501 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 ikilinganishwa na lengo la kutoa leseni 10,294.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma leo Mei 2, 2025 na Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde (MB) akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza Mheshimiwa Mavunde amesema leseni za uchimbaji zilizotolewa ni za uchimbaji mkubwa wa madini (SMLs) 1; leseni za uchimbaji wa kati wa madini (MLs) - 25; leseni za utafutaji wa madini (PLs) 396; leseni za uchimbaji mdogo (PMLs) ni 6,227
Aidha, amesema leseni kubwa za biashara (DLs) zilizotolewa ni 548; leseni ndogo za biashara (BLs) 1,290; leseni za uyeyushaji (RFLs) 1; na leseni za uchenjuaji wa madini (PCLs) 13.
Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, leseni 118 za utafutaji wa madini na leseni 41 za uchimbaji wa kati wa madini zilipewa hati za makosa kutokana na kutozingatia masharti ya leseni ikiwa ni pamoja na kutolipa ada za mwaka na kutoendeleza maeneo ya leseni.
Aidha, leseni tano za utafutaji madini na leseni tisa za uchimbaji wa kati zilifutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa hayo.
“Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo hadi kufikia Machi 2025 maeneo 65 yametengwa katika mikoa ya kimadini ikiwemo Geita, Mara, Mbogwe, Kahama, Chunya na Songwe,”amesema Mhe. Mavunde
Katika hatua nyingine, Waziri Mhe. Mavunde amesema sampuli 972 za makinikia ya Shaba zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi kutoka katika migodi ya Bulyanhulu Gold Mine, Katavi Mining Company Limited, Jiuxing (TZ) Mining Limited pamoja na ZEM (T) Company Limited.
Amesema, vilevile, sampuli 4,011 za wateja binafsi zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi lengo ni kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika uchimbaji na biashara ya Madini.
Mhe. Mavunde amesema pia, kutokana na uchunguzi huo, shilingi 296,732,000.00 zilikusanywa kama tozo stahiki za Serikali.


Post A Comment: