Na Amani Nsello- MBAGALA
Wagonjwa 251 wamepatiwa ushauri, elimu na tiba za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika kambi maalum ya afya bure Mbagala, Jijini Dar es Salaam.
Hayo yalibainishwa jana Mei 14, 2025 na Dkt. Bryson Mcharo, daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa mifupa wa watoto kutoka MOI.\n\nDkt. Mcharo alisema asilimia kubwa ya wagonjwa waliohudumiwa wanasumbuliwa na mifupa hususani wazee na kutoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya ya mifupa.
"Mpaka sasa tumeshaona na kutibu wagonjwa 251, kwa idadi hiyo wengi wao ni wale wenye umri mkubwa (wazee), kadri binadamu anavyokua na viungo vyake vinakuwa vinakosa ustahimilivu hivyo kupelekea matatizo ya mifupa" alisema Dkt. Mcharo
Pia, Dkt. Mcharo ametoa rai kwa wananchi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi na kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kuepuka na magonjwa ya mifupa.
Kwa upande wake, Bw. Joseph Mwakibinga mkazi wa Chamazi, aliwashukuru MOI na ATAPE kwa kuandaa kambi hiyo ya matibabu bure kwa wakazi wa Mbagala na viunga vyake na kuomba kambi za namna hiyo ziwe nyingi ili kwa wale wasiokuwa na uwezo wapate matibabu hayo.
Post A Comment: