*Bodi ya Wadhamini ya NSSF yaridhishwa na uwekezaji huo wa ubia na Jeshi la Magereza
Na MWANDISHI WETU,
Morogoro. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kudhihirisha mafanikio ya uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya viwanda kupitia mradi wa kimkakati wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichoko mkoani Morogoro, ambacho kimeanza rasmi uzalisha Julai 2024, kimezalisha ajira kwa Watanzania na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Mwamini Malemi, alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa ubia kati ya NSSF na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri, hongereni sana. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini tumejionea na tunathamini mnachokifanya,” alisema Bi. Mwamini mara baada ya kupokea taarifa ya Kiwanda kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), Bw. Selestine Some.
Kwa upande wake, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF alisema kupitia ziara hiyo ya kikazi, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wameweza kushuhudia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa mradi huo ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini.
Akisoma taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi Bw. Some alisema katika msimu wa mwaka 2024/25, kampuni ilipanga kuzalisha tani 20,000 za sukari ya majumbani, ambapo hadi mwisho wa msimu kiasi cha tani 19,124 sawa na asilimia 96 kilizalishwa.
Alisema pia, katika msimu wa 2025/26, Kampuni itaanza pia kuzalisha sukari ya viwandani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kiwanda,uliofanyika tarehe 8 Agosti 2024.
Bw. Some alisema uzalishaji wa sukari ya viwandani utapunguza uagizwaji wa bidhaa hiyo nje ya Nchi.
Alisema pia katika msimu wa uzalishaji wa sukari 2024/25 kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 2,172 na zisizo za moja kwa moja 8,000, na kuongeza biashara, shughuli za kiuchumi na kipato kwa Wananchi wa Mji wa Dakawa, Dumila na vijiji jirani.
MWISHO
Post A Comment: