NA EMMANUEL MBATILO, PWANI


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Mashariki limeteketeza bidhaa hafifu za vipodozi na nguo za ndani za mtumba tani 43 zenye thamani ya shilingi milioni 303 ambazo zimepigwa marufuku kuingia nchini.

Bidhaa hizo zilikamatwa katika operasheni waliyoifanya katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro na kubaini uwepo wa bidhaa hizo hatarishi.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Mei 2,2025 Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti wakati wa zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo katika Wilaya hiyo, amesema wafanyabiashara wanatakiwa kufuata utaratibu na sheria kuacha kuuza au kuagiza bidhaa ambazo hazikidhi viwango na ambazo zimepigwa marufuku kwani zinahatarisha afya ya mtumiaji na mazingira kwa ujumla.

Aidha DC Magoti ametoa rai kwa watu wenye dhamana ya ulinzi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weredi ili kuziba mianya ya upitishaji wa magendo wa bidhaa hizo kwa lengo la kulinda afya ya wananchi.

Pamoja na hayo amewapongeza TBS kwa kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuhakikisha bidhaa ambazo zinaingia na kuzalishwa nchini zinakidhi matakwa ya viwango ili watumiaji wa bidhaa wasiweze kupata madhara ya afya na mazingira.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TBS, Dkt. Kandida Shirima ameeleza kuwa wameamua kukataza avaaji wa nguo za ndani za mitumba ili kulinda utu na afya za wananchi kwani ni rahisi kusababisha maambukizi kwenye ngozi.

"Tunatoa wito kwa watu ambao huwa wananunua au wanatumia nguo za ndani za mitumba, tunaendelea kusisitiza kwamba waache kwani kutumia nguo za ndani za mitumba ni hatari kwa afya lakini pia inadhalilisha utu". Amesema

Sambamba na hayo Dkt Shirima ametoa wito kwa jamii kuacha matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu ambapo amesema vipodozi hivyo ni vile vilivyopigwa marufuku hivyo amewataka waache matumizi ya bidhaa hizo kwani zinaweza kusababisha athari kwenye ngozi.



Share To:

Post A Comment: