Lengo ni kumuwezesha mtoto wa kike kutimiza ndoto zake


DODOMA

Mei 29, 2025


IKIWA Tanzania leo inaungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani, Wizara ya Afya kupitia Mkurugenzi wa Kinga, Bi. Otilia Gowele, kwa niaba ya Waziri wa Afya Bi. Jensita Mhagama, imezindua Muongozo Mpya wa Hedhi Salama pamoja na nyenzo zake, zenye lengo la kumuwezesha mtoto wa kike kupata elimu bila vikwazo vinavyotokana na hedhi.


Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Bi. Gowele amesema kuwa muongozo huo mpya utakuwa ni nyenzo muhimu kwa shule, vituo vya afya, na jamii kwa ujumla katika kutoa elimu na huduma bora za hedhi salama kwa wasichana na wanawake nchini.


“Taarifa ya hali ya uchumi inaonyesha kuwa wanafunzi wa kike hupoteza masomo kutokana na changamoto za hedhi. Takriban asilimia 17 ya wasichana wameshindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa vifaa vya kujistiri au kuumwa wakati wa hedhi,” alisema Bi. Gowele.


Alitoa wito kwa jamii na wadau wote kutumia siku hii kama chachu ya mabadiliko, kwa kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata msaada na mazingira rafiki yatakayowawezesha kuhudhuria masomo kikamilifu hata wakati wa hedhi.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kinga, Bw. Joseph Birago, alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa maadhimisho haya mwaka 2015, kumekuwepo na mafanikio kadhaa katika uboreshaji wa mazingira ya hedhi kwa wasichana, ikiwemo ujenzi wa vyoo rafiki mashuleni, upatikanaji wa taulo salama za kike, na elimu kwa walimu na wanafunzi.


 “Lengo la siku hii ni kuondoa unyanyapaa na kuvunja ukimya kuhusu hedhi, huku tukihamasisha uwekezaji katika huduma bora na endelevu za afya ya hedhi,” alisema Bw. Birago.



Wizara ya Afya imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki yake ya msingi ya elimu bila vikwazo vya kiafya au kijamii.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: