Na, Egidia Vedasto, 

Serikalli kupitia Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi iko mbioni kutengeneza na kupitia upya sera na sheria mbalimbali itakaiyotambua Kada ya Miliki, Wathamini  pamoja na Madali nchini . 

Akizungumza Jijini Arusha katika mkutano wa 5 wa mwaka wa wadau  wa Miliki kuu nchini, Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Deogratius Ndejembi amewataka kuzingatia maadili  na maazimio  yatakayotolewa katika mkutano huo unaolenga kuimarisha Wizara hiyo  na kupanua wigo wa biashara nchini.

Aidha ameongeza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa wataalamu hao, unaolenga kukuza na kuimarisha miundombinu sambamba na kukuza uchumi wa nchi. 

"Mada hii ni ya kipekee kwa muktadha wa uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye nia thabiti ya kuleta mageuzi katika sekta ya makazi inayoendana na maboresho ya miundombinu, kama Reli ya Kisasa, maboresho ya barabara, usafiri wa anga na usafiri wa maji" ameeleza Ndejembi. 

Hata hivyo ameongeza kuwa, maendeleo ya nchi yanategemea sekta ya ardhi kwa asilimia kubwa, hivyo serikali itaendelea kushirikiana begabega na wataalamu wa miliki kuu ili kufikia malengo yanayotarajiwa. 

Kwa upande wake Rais wa chama cha wataalamu wa miliki kuu Tanzania ((AREPTA) Andrew Kato amesema kukosekana kwa sera ya makazi nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa sekta hiyo kutokaa vizuri kwa muda mrefu. 

Pia ameelezea umuhimu wa kutumia wataalamu katika ujenzi wa miradi mbalimbali nchini, hatua itakayosaidia miradi hiyo  kukamilika kwa wakati na kuwa katika mpango unaotakiwa. 

Amesisitiza umuhimu wa sera na sheria kuwa utasaidia kila mmoja kujua mipaka na taratibu zake, vivyo hivyo itawasaidia wananchi kuwaondolea mkanganyiko pale watakapohitaji huduma. 

"Katika mkutano huu muhimu tumeshirikiana na wenzetu wa Miliki Kuu kutoka Afrika mashariki, hii yote  ni kuhakikisha tunafikia malengo yetu kama jumuiya kwa pamoja" amesema Kato. 

Vile vile Makamu wa Rais wa Miliki Afrika Mashariki (AfRES) Prof. Nicky Nzioki amebainisha kuwa serikali inatakiwa kuiga kwa Nchi za Kenya na Rwanda katika namna bora ya kuboresha makazi nchini 

"Nina uhakika sera hii ikiwekwa na kutekelezwa kwa vitendo  basi hata idadi kubwa ya vijana nchini watapata ajira, si hivyo tu bali na uchumi wa nchi utakua kwa kasi", 

" Nakumbuka baada ya kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tulikuwa vizuri na ililenga kila mwananchi kuishi katika makazi bora, lakini baada ya shirika hilo kufifia, kila mmoja alianza kuwaza kuwa na kiwanja hali inayopelekea ujenzi  holela, nyumba sizizokamilika na wengine kujenga katika viwanja maeneo ya mafuriko, hii yote ni kwa sababu hakuna sera juu ya hilo" ameongeza Prof. Nzioki. 

Katika namna hiyohiyo ameiomba serikali kuweka mkazo katika sera ya makazi kama ilivyo katika sekta nyinginezo kama maji, umeme na afya. 

Mkutano huo umejumuisha Washiriki tatribani 180 wakiwemo Maafisa Ardhi, Watathmini, Wasimamizi na Watunzaji wa Majengo, Wawekezaji katika ujenzi, Wachambuzi wa uwekezaji katika sekta ya Miliki na Wataalamu wa Sekta Miliki na kubeba kaulimbiu "Matokeo ya Uboreshaji wa Miundombinu kwenye Upande wa Miliki Kuu Afrika Mashariki"

Share To:

Post A Comment: