MKUU wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amewataka viongozi na watumishi wa umma katika Mkoa huo kuhakikisha wanawatendea haki wanaowaongoza huku akieleza wazi hakuna sababu ya kutengenenezeaja ajali na kuumiza wengine.
Kihongosi ameyasema hayo alipokuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Mei Mosi wilayani Maswa Mkoani Simiyu ambapo tukio hilo limefanyika Kimkoa
“Niombe viongozi tuwatendee haki wenzetu pindi tunapopewa fursa ya kuongoza wengine ,asitokee mtu yeyote akamuumiza mtu na usiruhusu mtu akaharibikiwa ndani ya mikono yako .Usiruhusu kalamu yako ikamuonea mtu kumharibia maisha yake ya kazi.
“Viongozi tunawajibu mmoja kulea,kuelimisha,kuonya na kufundisha lakini kuwasaidia wale ambao wanachangamoto ili kuwa bora zaidi .Kwahiyo nitoe mwito ndani ya taasisi za umma ,halmashauri na maeneo mengine tuwatendee watu haki kama Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza.
“Itakuwa kosa kubwa sana endapo umepewa fursa ya kuongoza uoamuonea mtu tambua unaeneza laana kwako na kizazi chako,”amesema alipokuwa akitoa hotuba yake kwa wafanyakazi wa Mkoa huo.
Pia amesema wafanyakazi wanawajibu wa kuisadia nchi yetu pamoja na serikali yetu kwa kufanya Kazi kwa bidii lakini wakumbuke Taifa linawategemea na kufafanua wote ni mashahidi kuna watu maelfu kwa maelfu wanatamani kupata nafasi ambazo wamezipata wao lakini hawajapata hiyo fursa hiyo.
“Leo Mungu amekupa fursa hii itumie vizuri kwa ajili ya watu, fanya kazi bila kuchoka pale kwenye changamoto tuwasiliane ,viongozi wapo ili wananchi wanufaike na matunda ya Serikali yao.Kama wewe mganga mkuu wa Wilaya na kwenye hospital yako kukawa na malalamiko mengi maana yake unaigombanisha Serikali na wananchi.
“Kama ni Mkuu wa idara , mkuu wa kitengo au taasisi kukawa na malalamiko maana yake utendaji kazi utashuka na utendaji ukishuka wananchi wataishutumu Serikali lakini Serikali imekupa fursa ya kuwatumikia wananchi.
“Niombe sana kwa dhati ya moyo wangu kila aliyepewa kipande cha kwenda kufanya kazi akaifanye hiyo kazi bila kumpendelea mtu, bila kumuonea mtu na tujue kazi tulizonazo ni za muda utaondoka atakuja mwingine.
“Hivyo tuifanye kazi kwa uadilifu, mimi leo ni Mkuu wa mkoa na kabla sijaja alikuwepo mkuu wa mkoa maana yake nitaondoka na atakuja mwingine na hivyo hivyo kwa nafasi nyingine .Nafasi hiyo hutakuwa nayo milele,muombe Mungu akupe hekima,tumikia watu ili upate baraka kwa midomo itakavyokuwa inataja jina lako.”
Kihongosi amesema wakizingatia hayo watakuwa na Mkoa bora ,watakuwa watumishi bora zaidi na kwamba maeneo mengi ya kazi kumekuwepo na vitu haviko sawa. Kuna baadhi ya watu wanatabia ya kutengeneza chuki ndani ya viongozi na watumishi.
“Tabia ya kutengeneza majungu, uchonganishi ,uongo na kuwatengenezea wenzao ajali waonekane bora na wenzao waharibikiwe ,hatuna sababu ya kuumizana,matamanio yetu wote tuwe bora.
Ndio maana wakati nimekuja nilisema sitaki mtu yoyote aniletee habari ya Mtu mwingine bali nitazijua mwenyewe kwa kufanya naye kazi.
"Kwanini nasema hivi nimeshuhudia watu wengi wakiumizwa kwasababu ya midomo ya watu,watu wengi wanaonewa kwasababu hawana sauti ya kujitetea ,watu wengi wanaimiza kwa kutengeneza fitna hapa kati kati .Niombe viongozi na watumishi tutendeane haki , tupeane nafasi ya kusikilizana, tuangalie Utu ni jambo la msingi sana.”
Post A Comment: