Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Taasisi Mkoani humo kuweka utaratibu wa kufanya tathmini za Kiutendaji na amewapongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kuweka utaratibu wa kuwa na vikao vya aina hiyo ikiwa lengo ni kutathmini utekelezaji wa majukumu yao kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Ametoa rai hiyo leo Mei 02, 2025 alipokuwa akifungua kikao cha tathmini ya Utendaji kazi ya Mwaka ya RUWASA na amebainisha kuwa kikao hicho ni muhimu kwani kinatoa fursa ya kutathmini mafanikio, changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa huduma zinafika kwa wananchi wote.
“Nawapongeza sana kwa utaratibu huu wa kukutana kila mwaka na kujadili mafanikio yenu pamoja na changamoto zilizojitokeza na kupanga suluhisho la kuzitatua, natoa wito pia kwa Taasisi zingine”. Mhe. Mtanda.
Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa wa Mwanza umeshuhudia mageuzi makubwa katika sekta ya maji vijijini, kwa juhudi na uwekezaji wa Serikali imefanikisha kuboresha maisha ya watu kupitia utekelezaji wa miradi ya maji 78 ambayo tayari imekamilika, na miradi 70 inaendelea kutekelezwa.
Kadhalika Mhe. Mtanda amesema Kabla ya kuanzishwa kwa RUWASA mwaka 2019, kiwango cha wananchi waliokuwa wakipata huduma ya maji vijijini kilikuwa ni asilimia 45 pekee lakini leo hii kutokana na juhudi hizo kiwango hicho kimepanda hadi asilimia 82.8 wananchi waliofikiwa na miundombinu ya Maji Vijijini.
“Hili ni jambo la kujivunia, na ni ushahidi kuwa tupo kwenye njia sahihi ya kumtua mama ndoo kichwani na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 inayotaka kufikisha huduma ya maji vijijini kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025”
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Godfrey Sanga amesema wamekuwa na utaratibu huo wa kukutana na Watumishi kila mwaka wakilenga kujadili masuala mbalimbali ya kitendaji, Sambamba na hayo Mhandisi Sanga amesema katika kikao hicho mada mbalimbali za kujengeana uwezo kama vile Rushwa, Utumishi wa Umma, Elimu ya Afya ya Akili pamoja na kusomeana Taswira ha Bajeti zitajadiliwa.
Post A Comment: