Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda akiwa kwenye Kijiji cha Tukusi Wilayani Monduli Mkoani Arusha, amezindua Mpango wa uchimbaji Visima virefu zaidi ya 30 kwenye Majimbo yote ya Mkoani Arusha ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na maji ya uhakika, salama na safi muda wote.

Katika uzinduzi huo, Wizara ya Maji kupitia kwa Bw. Gibson Bayona, Mratibu wa Kampeni ya Maji inayoendelea nchi nzima ya "Maji Mwa Mwa Mwaa", amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatokana na uwezeshaji wa serikali ya awamu ya sita uliotokana na fedha za kupambana na janga la UVIKO-19, ambapo fedha zake zilitumika kununua mitambo 25 ya uchimbaji wa visima virefu na utengenezaji wa mabwawa ya maji kwenye mikoa zaidi ya 25 ikiwemo mkoa wa Arusha.

Kwa upande wao wananchi wanufaika wa mradi huo wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka, wakimuombea kheri, afya njema na uwajibikaji mwema katika majukumu yake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja naye Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda kwa kuweza kuwafikia na kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani hapa.



























Share To:

Post A Comment: