Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb)imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajenda yake ya kukuza utalii ikiwemo katika miradi ya ujenzi wa kituo cha utalii kwa gharama ya shilingi bilioni 21.4 na kituo cha utafiti kwa shilingi bilioni 1.55 chini ya mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), Kihesa Kilolo Mkoani Iringa.
Ameyasema hayo leo Septemba 7, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika miradi hiyo mkoani Iringa.
“Kwa ujumla kama Kamati tunaendelea kuipongeza Serikali, kumpongeza Rais Samia kwa namna ambavyo anaendelea kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za nchi yetu ikiwemo ajenda yake kubwa ya kukuza utalii” amesisitiza Mhe. Mnzava.
Amefafanua kuwa kamati imeishauri Serikali kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa wakati ambapo kwa upande wa Kituo cha utafiti amesema sehemu kubwa ya kazi ya ujenzi wa kituo hicho inakwenda vizuri huku akimuelekeza mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha utalii kutimiza wajibu wake ili kukamilisha kazi hiyo.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha za miradi hiyo huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia miradi hiyo itekelezwe kwa wakati.
Mhe. Chana ametoa rai kwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia mikataba yao na kukamilisha miradi kwa wakati.
“Nitoe angalizo kwa Wakandarasi walio kwenye miradi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni muhimu sana kutekeleza miradi kutokana na mikataba tuliyowekeana ili ikamilike kwa wakati” amesema.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utaklii iko Mkoani Iringa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Post A Comment: