Na Mariam Kagenda _Kagera


Wadau mbalimbali  halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera wamekutana pamoja kujadili jinsi ya kuongeza bidii katika suala la kupambana na changamoto ya udumavu na utapiamlo kwa wananchi.


Wadau hao kutoka maeneo tofauti tofauti wamekutana  Julai 4, 2024 katika kikao kazi cha lishe kikilenga zaidi taathimini ya utekelezaji wa mradi walishe uliokuwa ukitekelezwa na Shirika la PANITA   kilichofanyika Manispaa ya Bukoba ambapo katika majadiliano hayo suala la elimu ya lishe limebainika kuwa  bado ni changamoto inayowakabili  wananchi walio wengi. 


Wamefafanua kuwa kutokana na jamii kuwa na uelewa mdogo juu ya ulaji  wa  vyakula mchanganyiko na vyenye virutubishi  imepelekea baadhi ya  wananchi kutokukubali kubadilika  nakuendelea kutumia vyakula kwa mazoea ambapo wametoa mfano  jamii inavyokula chakula aina ya ndizi kwa  wingi bila ya mchangayiko wa chakula kingine.


Joseph matope  ni kaimu afisa elimu  awali na msingi wilaya  amesema kuwa Bukoba na Kagera kwa ujumla vyakula vipo vya kutosha lakini matumizi yamekuwa  ni hafifu mno.


"Vyakula wanavyo magimbi yapo, maharage yapo, mboga za majani zipo, mihogo na vingine vingi vipo lakini hawavichanganyi wakati wa ulaji, watoto wanawapa ndizi pekee kuanzia asubuhi, mchana na kuendelea, tubadilike wote ili kuyafikia malengo, amesema  afisa Joseph Matope"


Afisa huyo pia ameeleza kuwa  sekta ya elimu  jitihada zimefanyika nakuhakikisha shule nyingi  halmashauri hiyo zinatoa huduma ya uji na  chakula kwa wanafunzi japo shule zinazotumia unga uliorutubishwa ni chache kutokana na mashine zinazosindika unga wa lishe kuwa chache maeneo ya Bukoba. 

 

Jambo jingine lililoelezwa   kuchochea udumavu nipamoja na baadhi ya wazazi   kutokuwa tayari kupokea maelekezo muhimu kutoka kwa watalaamu wa afya juu ya utekelezaji  wa  lishe, maelezo ambayo yametolewa  naye mwalimu Paschal Ngaiza.


"Tunapolisimamia  suala hili  la lishe tujitowe ufahamu wazazi hawa  wengine ni  wakorofi wamekuwa wagumu hata kuchangia chakula cha watoto shuleni, hii lishe imekuwa   pasua kichwa kwa hiyo tunatakiwa wote kujikakamua na kujipanga vilivyo kuibadilisha jamii yetu hii" mwalimu Paskal akisisitiza.


Hata hivyo kwa upande wao PANITA ambao ni mwavuli wa mashirika ya kijamii yanayoshughulika na masuala ya afya  na lishe kwa kushirikiana na Gain pamoja  na  Sanku wanaotekeleza mradi  wa urutubishaji chakula shuleni kupitia Afisa mradi Lubango Charles wamezitaja shughuli za miradi  ya lishe zilizoteketezwa   kwa Bukoba  DC ikiwemo ya kukutana na viongozi wa halmashauri na wadau wa lishe, kukutana na viongozi wa kata hasa kata  ya Kemondo, kuhamasisha  uanzishwaji wa bustani za mbogamboga shuleni, wamezifikia  shule tano, wamewajengea uwezo watalaamu wa afya ngazi ya jamii, kuelimisha jamii matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa, usimamizi shirikishi katika utekelezaji wa maazimio ya mradi na nyinginezo.


Akihitimisha taarifa Afisa Lubango  amesema mradi huo kwa sasa umefika kikomo, hivyo ametoa wito akiwasihi wadau wote kupitia nyadhifa zao kujimudu na kuibeba kwa dhati dhana nzima ya  lishe kwa kuifuatilia jamii  ili kuona kama yanayoelimishwa  yanatekezwa kwa ufanisi.


Kaimu afisa  lishe  wilaya Donald Kalenzo  amebainisha na kusema kuwa   lishe bora ni jambo ambalo limekuwa likipambaniwa zaidi  katika halmashauri ya  Bukoba   ili kuhakikisha udumavu na utapiamlo unapungua kwa kiwango kikubwa na jamii ibakie kuwa salama kama yalivyo makusudi ya serikali.


Amewahimiza wadau wote kuungana  pamoja  kuupiga vita udumavu ili kuwalinda watu wote  nakuwa na jamii yenye lishe bora  kuanzia  wanawake wajawazito na  watoto.


Joanitha Jovin ni afisa lishe mkoa akipongeza juhudi za PANITA kwa kazi kubwa waliyoifanya Kagera amewakumbusha wadau kuwa udumavu ni adui ambaye anapaswa kutokomezwa ili kuinua afya ya jamii kwani Kagera ni mkoa wenye neema ya vyakula hivyo haina sababu ya kuwa katika hali ya udumavu kama ilivyo kwa sasa.


Licha ya pongezi na shukrani ametoa ombi kwa shirika hilo kurejea tena Kagera  kwa miradi mingine ya lishe ili kuzifikia wilaya zote za mkoa kwani awamu   hii ilizihusisha halmashauri  tatu  za  Bukoba  DC, Manispaa ya Bukoba na  Muleba. 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: