Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amepiga marufuku hospitali za Mkoa wa Arusha kuzuia maiti kutokana na gharama za matibabu na badala yake zibuni njia mbadala za kudai malipo hayo.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda ametoa katazo hilo leo Mei 27, 2024 alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli kukagua maendeleo ya Ujenzi wa jengo la mionzi na la upasuaji pamoja na kuzungumza na wahudumu wa hospitali hiyo na kuangalia namna huduma zinavyotolewa hospitalini hapo.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa na Waganga wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha kusimamia agizo hilo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa kupitia kwa Waziri wa afya.

Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha akiwa Hospitalini hapo amewataka wahudumu wa afya mkoani Arusha kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanaofika hospitalini na kwenye vituo vyote vya afya ili kuwa sehemu ya kuwapunguzia maumivu wananchi kutokana na magonjwa yanayowasumbua.

Mhe. Makonda amesema Mkoa wa Arusha unafaa kuwa Mfano wa huduma nzuri za afya ili kuendana na uwekezaji mkubwa wa serikali ya awamu ya sita kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi za kuwezesha miundombinu bora ya utoaji wa huduma za kiafya.

Mhe. Paul Makonda anaendelea na ziara yake ya Kikazi Wilayani Monduli ambapo pamoja na mambo mengine amepangiwa pia kukagua mradi wa maji wa Kijiji cha NAFCO kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufanyika eneo la Meserani maarufu kama Duka bovu.
Share To:

Post A Comment: