Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Rutahengerwa amesema ili kuwa na uhai lazima jamii izingatie suala la hedhi salama kwa watoto kike na wanawake.

Rutahengerwa amesema hayo leo Mei 25, 2024 jijini Arusha wakati wa hafla ya ufunguzi wa juma la Hedhi Salama nchini ambapo kilele chake kitafikia Mei 28, 2024 mwaka huu.

Akiongea katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha, Mhe. Rutahengerwa amesema ni jukumu la wake kwa waume kuungana kuhakikisha mwanamke anakuwa na hedhi Salama.  

"Takwimu zinaonesha kwamba takriban wanawake milion 13.7 nchini wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 ambao kimsingi huwezi kupata hedhi kila siku,hivyo jamii inatakiwa kuweka mazingira wezeshi kwa mwanamke ili apate hedhi salama "Amesema mhe. Rutahengerwa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mratibu wa masuala ya Hedhi salama taifa, Bi. Mariam Mashimba kutoka Wizara ya Afya amesema hedhi salama ni suala linalowezekana.

"Tunaposema hedhi salama ni hatua ya Wanawake na Wasichana kupata elimu sahihi kuhusu hedhi hivyo watumie siku za juma la hedhi salama kufika viwanja hivyo vya Makumbusho Arusha kupata elimu kutoka kwa wataalam wa afya watakaokuwepo hapo". Amesema Mariam.

Mariam amesema, suala la hedhi hutofautiana baina ya mtu na mtu na hii huweza kusababishwa na suala la lishe hivyo kila msichana au mwanamke lazima kuwa na uelewa sahihi wa hedhi na namna ya kuweza kujihudumia.

Kwa upande wake Katibu wa Jukwaa la Hedhi salama nchini Bw. Severine Alutte amesema, wanawake ni lazima wazingatie matumizi sahihi ya taulo za kike.

"Ukweli ni kwamba, taulo za kike zinaweza kuleta changamoto lakini pia matumizi yasiyo sahihi ya taulo yanaweza kusababisha madhara hivyo, kila mwanamke ni vema kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha taulo wanazo tumia zimehakikiwa na Mamlaka ya Chakula nchini pamoja na Shirika la viwango nchini TBS" amesema Allute.

Allute amewataka wanawake na wasichana kuhakikisha wanakuwa na matumizi sahihi wanapotumia taulo hizo kwa muda uliopangwa kulingana na hali ya hedhi, huku akisisitiza kuzingatia usafi wakati wote.

Wakati wa ufunguzi wa  maadhimisho yamefanyika matembezi ya km.5 ikiwa ni njia moja wapo yakutoa elimu ya hedhi salama.

Share To:

Post A Comment: