Kampuni ya Multicable Limited inayojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za Umeme pamoja na masuala ya utalii imekabidhi Pikipiki 10 kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Christian Makonda katika jitihada za Kuimarisha Ulinzi na usalama Mkoani Arusha pamoja na kukuza Utalii wa Arusha.

Pikipiki hizo zimekabidhiwa leo Jumamosi Mei 25, 2025 kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Hussein Ali Bhai na Murtaza Ali Bhai ambao ni Wakurugenzi wa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Jijini Dar Es Salaam ikifanya kazi kwenye majiji yote ya Tanzania bara.

Bw. Hussein Bhai amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa kuendelea kuimarisha suala la ulinzi na usalama Mkoani Arusha na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Mkoa wa Arusha katika kuharakisha maendeleo ya wakazi wa Arusha na Mkoa kwa Ujumla.

"Sisi Multcable Limited tumekuja kuunga juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika kampeni yake ya kuufanya Mkoa kuwa sehemu salama.Tumeona utendaji wake katika kulisaidia Jeshi la Polisi kufanya shughuli zake na tunaahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi yake." Ameongeza kusema Bw. Hussein.

Kwa upande wake Mhe. Paul Christian Makonda amesema kukamilika kwa ahadi yake hiyo kwa Jeshi la Polisi ya  kuwapatia Jeshi hilo Pikipiki 50 ni muendelezo wa hatua nyingine ya kuwatafutia Pikipiki za Umeme 100 pamoja na magari 20 kwaajili ya kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika jitihada za kuendelea kukuza na kuimarisha utalii na uwekezaji mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda amesema lengo lake ni kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa ufanisi kwa kuwa na vifaa vya kisasa na vya kutosha vitakavyowawezesha kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu kabla haujatokea ili kulifanya Jiji la Arusha kuwa kivutio cha wageni na watalii wanaofika  kufanya utalii na shughuli mbalimbali.

Mkoa wa Arusha unaoongozwa na Mhe. Paul Christian Makonda ni kitovu cha Utalii wa Kaskazini mwa Tanzania na ndio Mkoa unaotambulika kama Mkoa wa kidiplomasia kutokana na kuwa na mikutano na ofisi nyingi za kimataifa pamoja na kuwa lango la kuelekea kwenye hifadhi na mbuga kubwa za wanyama zilizopo nchini Tanzania ikiwemo Hifadhi ya Ngorongoro.

Share To:

JOEL MADUKA

Post A Comment: