Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na taratibu za uwekezaji kwa kuongeza vituo vingine 4 kwa kujenga majengo na kuviwezesha vifaa vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa Saratani kwa njia ya mionzi.
Waziri Ummy amesema hayo leo Aprili 5,2024 kwenye Bunge la 12, Mkutano wa 15, Kikao cha Nne wakati akijibu swali namba 6,133 kutoka kwa Mbunge wa Vito Maalum Mhe. Tunza Issa Malapo aliyeuliza ‘Je ni Hospitali ngapi zinatoa huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani hapa nchini.
Amesema, kwa sasa Serikali ina jumla ya vituo Vinne ambavyo vinatoa huduma ya matibabu ya Saratani nchini kwa njia ya Mionzi, vituo hivyo ni Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Kanda Bugando, Hospitali ya binafsi Besta na Hospitali ya Good Sammaritan (St. Fransis Ifakara).
“Serikali inaendelea na taratibu za uwekezaji kwa kuongeza vituo vingine 4 kwa Tanzania Bara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali binafsi ya Agakhan) na kimoja kwa Visiwani Zanzibar (Hospitali ya Binguni) kwa kujenga majengo na kuviwezesha vifaa vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa Saratani kwa njia ya mionzi.” Amesema Waziri Ummy
Wakati akijibu maswali ya nyongeza Waziri Ummy amesema Serikali imejipanga kukamilisha kwanza Hospitali ya Kanda ya Mbeya kwa kuwa ina Mkoa mingi (Katavi, Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe) ambayo ina watu wengi zaidi ya Milioni 15 ambao wanasafiri hadi Ocean Road kwa ajili ya kufata huduma za Saratani kwa njia ya mionzi.
Swala la elimu, Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kutumia njia mbalimbali kuendelea kutoa elimu ili wananchi wajitokeze kupima Saratani kwa kuwa takwimu zinaonesha kila Mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani Elfu 40 na wanaofika kwa ajili ya kupata huduma ni asilimia 30.
“Na hao wanaokwenda Hospitali kupata huduma asilimia 70 wanafika wakati tayari Saratani ikiwa katika hatua ya Tatu na hatua ya Nne ambayo inakua ni ngumu kutibu au matibabu kuchukua mda mrefu, tujitokeze kupima Saratani kwa kuwa Saratani inatibika ikigunduliwa mapema.” Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy amewataka Waganga Wafawidhi wa vituo vyote vya kutoa huduma za Afya nchini vya Serikali, kutenga angalau siku Moja kwa kila Mwezi ya watu kupima Saratani na Madaktari wa Mikoa na Wilaya wasimamie maelekezo hayo ya Serikali.
Post A Comment: