WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kiongozi yeyote katika mamlaka za serikali za mitaa atakayebainika kuunda kikundi hewa kwa lengo la kujifaidisha na fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya vikundi awe Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya atakuwa amejifukuzisha kazi.


Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Rufiji mkoani Pwani kuhusu mwekezaji wa mradi wa sukari ambaye ameshindwa kutimiza ahadi ya kuwalipa fidia baadhi ya wakazi wa ene lililogawiwa kwa mwekezaji huyo.

Alisema baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia kurejeshwa kwa mikopo ya asilimia 10 ya vikundi hatarajii kuona ubadhirifu wa aina yoyote wa fedha hizo, wenye sura ya ushiriki wa viongozi ndani yake.

“Kwenye hili la mikopo ya asilimia 10 nalirudia mara tatu tatu, ni hivi! kiongozi yeyote awe Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya au yeyote katika ofisi hizi atakayethubutu kushiriki kwenye kuandaa vikundi hewa ili aweze kujipata fedha hizi za mikopo, nasema hivi hana kazi.”

 “Nyote si mmesikia kuhusu ripoti ya CAG, watu walikuwa wanaanda vikundi hewa mpaka viongozi wa juu wa mikoa na wilaya wanashiriki kwenye uandaaji wa vikundi hivyo,  alafu wanachukua hela za mikopo ya watu wa makundi maalum, ni aibu kwa kiongozi kushiriki kwenye ubadhirifu wa fedha, tena zilizotengwa kuwawezesha wahitaji katika makundi maalum”.

Amesema baada ya Rais Samia kuridhia urejeshwaji wa mikopo hiyo, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea na ukamilishwaji wa taratibu zitakazotumika katika ukopeshaji wa vikundi hivyo ili kuhakikisha fedha hizo zinakopeshwa kwa walengwa tu.

“Hivi karibuni tutaanza kutoa mikopo hiyo na kwa sasa ofisi yangu inaendela na ukamilishwaji wa kanuni na taratibu za mwisho kabisa, ila nawaonya, fedha hizi tunataka ziwafikie walengwa na ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia.”

“Hivyo yeyote atakayejaribu kuzigusa huyo anajaribu kunikwamisha nawaahidi nitashughulika naye,” alisema Waziri Mchengerwa.

Kuhusu vikundi ambavyo bado havijamaliza marejesho ya mikopo hiyo, Waziri Mchengerwa amesema lazima virejeshe fedha hiyo ya serikali na katika hilo wahusika lazima wawajibishwe ili fedha hiyo irudi.

Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amewataka wakuu wa shule kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji na mitaa kufanya mikutano ya mara kwa mara pindi wanapotaka kuweka michango shuleni ili kuwashirikisha wananchi na wawashawishi waridhie michango hiyo.

“Kwenye hili la michango nasema hivi, walimu msiwachangishe michango wazazi ambayo hamjawashirikisha wala hawajaridhia, fanyeni mikutano mingi muwezavyo washirikishe juu ya umuhimu wa michango mnayoitaka na waridhie kwa Pamojakwa ajili ya maendeleo ya Watoto wao na jamii nzima kwa ujumla”.
Share To:

Post A Comment: