Ikiwa ni mwendelezo wa ziara za kutembelea Kampasi zote tangu kuthibitishwa katika nafasi yake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha April 29 akiwa ameambatana na baadhi ya Wajumbe wa timu ya Menenjimenti, amekutana na Wafanyakazi wa chuo hicho katika Ndaki ya Dar es Salaam kwa lengo la kujadiliana masuala ya maendeleo ya chuo ambapo ameweka bayana vipaumbele katika uongozi wake.

Prof. Mwegoha amewahimiza Wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na Menejimenti kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya Mpango Mkakati wa Tano wa chuo yanafikiwa huku akitaja vipaumbele vyake katika utekelezaji kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa chuo kinajulikana  zaidi ndani ya nchi na kimataifa pamoja na kuanzisha ushirikiano na vyuo mbalimbali duniani na kuongeza idadi ya Wanafunzi hasa wa shahada za uzamili (Postgradraduate).

Ametaja vipaumbele  vingine kuwa ni kuhakikisha Wafanyakazi wenye sifa na vigezo vya kitaaluma wanapanda vyeo kwa wingi na kwa wakati, kufanya uwekezaji mkubwa na kuongeza mapato ya ndani, kuboresha miundombinu ya chuo na mazingira ya kufundishia pamoja na kuanzisha mifumo itakayorahisisha utendaji kwa kila taasisi,idara na vitengo ndani ya chuo.

Ameongeza kuwa sambamba na pongezi nyingi za kuthibitishwa kwake kutoka kwa Wafanyakazi wenzake,  amesisitiza kwamba atasikia fahari zaidi endapo pongezi hizo zitaambatana na ufanisi wa hali ya juu kwa Wafanyakazi wote utakaoleta mabadiliko na mapinduzi makubwa ya kimaendeleo kwa chuo hicho ndani ya miaka mitano ya uongozi wake.

Katika kuhakikisha chuo kinaongeza muonekano wake na kujulikana zaidi kimataifa katika nyanja za kitaaluma, Prof. Mwegoha amewataka Wanataaluma wote kujisajili katika mtandao wa wanataaluma wa kidunia (Google scholars), kuongeza idadi ya machapisho yenye uwezo wa kufanyiwa marejeo kwa wingi (citations) na kila taasisi ndani ya chuo kuandaa dhima na dira zao zinazoendana na mpango mkakati wa chuo ambazo zitasaidia kuwaongoza kiutendaji ndani ya miaka mitano.

Katika hatua nyingine Wafanyakazi hao wamepongeza kasi ya utendaji wake pamoja na Menejimenti nzima na kuongeza kuwa matokeo chanya yameanza kuonekana ndani ya muda mfupi ikiwemo kupanda vyeo kwa Wanataaluma wengi hadi kufikia ngazi ya uprofesa jambo ambalo lilikuwa gumu hapo awali.

“ Sisi tunakupongeza sana kwani ndani ya muda mfupi wa uongozi wako tumeona  mafanikio makubwa ikiwemo ya kupanda vyeo kwa Wanataaluma wengi  kwa haraka, kupata Viongozi kamili, kumaliza tatizo la umeme na mtandao pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo”. Alisema Prof. Cyriacus Binamungu,  Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam.

Share To:

Post A Comment: