Jopo la Wataalamu kutoka sekta ya utalii nchini Morocco na jopo la wataalamu wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini wamekutana na kufanya mazungumzo yaliolenga kuimarisha ushirikiano katika kutoa huduma bora za utalii pamoja na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na Morocco.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho mapema hivi leo, Naibu Balozi wa Morrocco nchini Lahoucine Rahmouni alisema ujumbe wa wataalamu watatu kutoka Morocco uliwasili nchini aprili 28, 2024 tayari kujadili kuhusu namna bora ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania nchi yake katika sekta ya utalii.
Balozi Rahmouni anasema ujumbe huo unajumuisha Mkuu wa Idara ya Ushirikiano katika Wizara ya Utalii, Utamaduni, Uchumi wa Jamii na Ushirikiano, Omar Dinia, Mkuu wa Idara ya Sheria na Ubora katika Wizara ya Utalii, Utamaduni, Uchumi wa Jamii na Ushirikiano, Zineb Saidi na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Kitaifa ya Utalii ya Morocco, Sarah Benabdellah.
“Nimepokea jopo la wataalamu kutoka Morocco watakaokuwa nchini hadi Mei 3, 2024 wakihakikisha wanafanya majadiliano ya kina na wataalamu wa Sekta ya Utalii nchini ili kuona namna gani nchi hizi mbili zinaweza kushirikiana katika eneo ya mafunzo ya watoa huduma za utalii, eneo la uhusiano kwa umma na utangazaji ili pande zote zinufaike,” anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB), Ephraim Balozi Mafuru anasema ujio wa wajumbe hao unafungua fursa mpya ya kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini na kuboresha huduma za utalii ili wageni wa ndani na nje ya nchi waweze kuvifikia vivutio hivyo.
"Rais Samia Suluhu Hassan ametuheshimisha kama nchi kupitia Filamu maarufu ya Royal tour, watalii wanamiminika nchini sasa ni muda muafaka wa kufikiria nini tunafanya kuendeleza jitihada za mama, mkutano huu ni moja ya mikakati ya nchi kuhakikisha sekta ya utalii na uwekezaji unakuwa nchini, tutaitumia ipasavyo,” anasema.
Ujio wa wataalamu hao toka Morocco ni matokeo ya mkutano uliofanyika Rabat, Morocco, kati ya Mhe. January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kiafrika na Wamorocco wanaoishi Nje, Mhe. Naser Bourita katika siku za karibuni.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Chuo cha Utalii Tanzania (NCT) Makumbusho ya Taifa ( NMT) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Post A Comment: