Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema mahitaji na matumizi ya baruti kwa sasa yameongezeka kutokana na kuimarika kwa shughuli za uchimbaji wa madini na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Waziri Mavunde ameyamesema hayo leo Aprili 30,2024 Bungeni Jijini wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuongeza kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, vibali 252 vya kuingiza, kupitisha, kutengeneza na kuuza baruti nchini pamoja na vibali vya kusafirisha baruti nje ya nchi vimetolewa.
“Fedha zilizopatikana kupitia utolewaji wa vibali hivyo ni jumla ya dola za Marekani 126,600, ameongeza Wizara ilitoa vibali nane (8) kwa ajili ya utengenezaji wa baruti aina ya emulsion kwa kutumia gari za Mobile Manufacturing Unit (MMU) kati ya vibali hivyo, saba (7) vilitolewa kwa Kampuni ya Orica Tanzania Limited na kibali kimoja (1) kwa Kampuni ya Dangote Cement Limited ambavyo vitatumika kwa muda wa miaka miwili.
Aidha ameongeza kuwa Wizara ilifanya ukaguzi kwenye maeneo yaliyoombewa kujengwa maghala ya kuhifadhi baruti ambapo maeneo yaliyofanyiwa ukaguzi ni Saleni–Pwani, Manyoni na Itigi–Singida, Kahama na Bushimangila–Shinyanga na Eneo Tengefu la Mirerani–Manyara.
Ukaguzi huo ulibaini kuwa maeneo hayo yalikidhi matakwa ya Sheria ya Baruti, Sura ya 45 na hivyo kupewa vibali vya ujenzi wa maghala ya kuhifadhi baruti.
Post A Comment: