Na Dickson Mnzava, Same.


Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela Said Ramadhani Mshana miaka 45 mpare mfanyabiashara na mkazi wa masandare wilayani Same Mkoani Kilimanjaro baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kijangili.


Miongoni mwa makosa ambayo amekutwa nayo mshitakiwa huyo ni pamoja na kukamatwa na nyara za serikali kinyume cha sheria na kujihusisha na ujangili wa nyara za serikali.


Akitoa hukumu hiyo tarehe 18 April 2024 hakimu mkazi Mkuu mahakama ya Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro mheshimiwa Chrisanta Chitanda amesema mshitakiwa alikamatwa katika eneo la kandoto Kata ya kisima wilayani Same Mkoani Kilimanjaro akiwa na meno 6 ya tembo yenye uzito wa kg 33 na thamani yake ni 105,255,000 pesa za kitanzania sawa na USD 45000.


Awali mwendesha mashitaka wa hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA)Ndugu Samweli Magoko amesema mnamo tarehe 28/02/2023 katika eneo la kandoto Kata ya kisima wilayani Same mshitakiwa alikamatwa na maafisa wanyama pori baada ya kumuwekea mtego mshitakiwa kuwa wao wananunua meno ya tembo ndipo mtu huyo alipo jitokeza na kusema anauza meno hayo ya tembo.


Magoko aliiomba mahakama hiyo ya wilayani Same kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kwani makosa aliyotenda mshitakiwa huyo kwa mujibu wa sheria ni makosa ya kuhuju uchumi na yanafubaza jitihada za serikali katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Nchi kwa manufaa ya watanzania wote.


Kufuatia ushahidi huo ulitolewa na jamuhuri mahakamani hapo dhidi ya mshitakiwa huyo mahakama iliweza kumkuta na hatia ya kuhujumu uchumi na kosa la ujangili bwana Said Ramadhani Mshana hivyo hakimu mkazi mkuu mheshimiwa Chrisanta Chitanda kumhukum kwenda jela miaka 20 kwa kosa la kwanza la kukutwa na nyara za serikali kinyume na kifungu cha sheria namba 86(1)(2)(c) sura ya 283 marejeo ya mwaka 2022 sheria ya uhifadhi wa wanyama pori.


Mshitakiwa huyo pia amekutwa na kosa la pili la kujihusisha na nyara za serikali kinyume na kifungu cha 84(1) cha sheria ya uhifadhi wanyama pori sura ya 283 marejeo ya mwaka 2022 hivyo mahakama hiyo kumhukum tena mshitakiwa huyo kwenda jela miaka 20 ambapo adhabu hizo atazitumikia kwa wakati mmoja.


Mshitakiwa amekutwa na kesi ya kuhujumu uchumi namba 5/2023 shauri la uhujumu uchumi Na.5/2023.


Akizungumza nje ya mahakama hiyo Mkuu wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa Mkomazi Kamishina msaidizi wa uhifadhi Emmanuel Moirana ametoa rai kwa wananchi wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wa namna hii kuacha mara moja kwani jeshi la uhifadhi kupitia kitengo cha intelejesia na upelelezi vimejipanga kukabiliana na uhalifu wowote wa nyara unaotokea ndani na nje ya Hifadhi.


Moirana amesema uhalifu wa namna hii unadidimiza jitihada za mheshimiwa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kukuza utalii Nchini.


 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: