WANANCHI wa Jimbo la Moshi vijijini mkoa wa Kilimanjaro wameendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za mfuko wa Mbunge wa jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, barabara na afya.

Akizungumza mara baada ya kikao cha kujadili maendeleo ya mfuko wa Jimbo na kugawa fedha walizopokea kutoka serikali kuu zaidi ya milioni 74, Mbunge wa Jimbo hilo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amesema miradi inaendelea katika kata husika.

Profesa Ndakidemi alisema maendeleo ya miradi ambayo walipangia kazi mwaka jana ambazo zilishaanza ikiwemo kurekebisha mifereji ya asili, umaliziaji wa ujenzi wa zahanati Kijiji cha Chemchem kata ya Arusha chini, zahanati ya Mvuleni kata ya Mabogini sambamba na kukagua miradi hiyo.

Amesema kata 14 zilitengewa fedha kwa ajili ya kurekebisha mifereji ya asili ambayo husaidia wananchi kupata huduma ya maji ya kumwagilia ili waweze kupata mazao mbogamboga, ndizi na kahawa ili waweze kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Pia alisema bajeti ya mwaka huu 2024 kata 15 ndiyo zilizoleta mahitaji ya miradi ya kutekeleza isipokua kata moja ya Mbokomu ambayo Diwani na Afisa Mtendaji hawakuleta mahitaji ambapo kila kata imetengewa zaidi ya shilingi milioni 4 zitakazotatua baadhi changamoto kwenye kata zao.

“Baadhi ya kata wamesharekebisha mifereji ambapo wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji ya kumwagilia, natoa wito kwa kata ambazo hazijarekebisha wahakikishe wanashughulikia ili huduma hiyo ipatikane” Alisema Profesa Ndakidemi

Luiza Mgungu ni Afisa mtendaji Kijiji cha Rau ulipo mradi wa mifereji wa kisarika namba moja alisema kuchelewa kukamikika kwa mradi ni kutokana na mvua huku akisema mbali na changamoto hiyo wananchi wanaendelea kujitoa kwa nguvu kazi zao ili kuunga mkono jitihada za serikali kupitia mfuko wa Mbunge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji cha Kirishi Kijiji cha Mrawi kata ya Uru kaskazini, Frank Msoka ulipo mradi wa mifereji wa tumbokisima alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kilimo cha umwagiliaji lakini pia utoshelevu wa huduma ya maji pamoja na kuzuia wadudu waharibifu shambani kama fuko.

“Kwa sasa wananchi wanaenda mjini kununua mboga badala wapeleke wao mjini hivyo ukikamilika huu mradi utasaidia wananchi wa Kijiji kata na hata jimbo kujikwamua kupitia kilimo cha umwagiliaji.” Alisema Msoka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi yawananchi watakaonufaika na miradi hiyo inayokarabatiwa na kuboreshwa walisema itawasaidia kufanya kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya barabara na afya.

Share To:

Post A Comment: