KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEM kwa kuja na mfumo wa ufundishaji mubashara na kusisitiza kuwa mfumo huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa dunia ya sasa ni ya kidigitali.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa LAAC, Mhe. Halima Mdee wakati Kamati hiyo ilipotembelea Shule ya Sekondari ya Dodoma ambaye alisema hatua ya kuja na mfumo huo umekuja wakati muafaka na utakabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu.

“Pongezi hizi ni kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu kwa niaba ya kamati yangu ya LAAC na wabunge, tuwapongeze sana katika hatua hii kwani dunia ya sasa ni ya kidigitali.”

“Ni ukweli usiopingika kuwa kuna pengo kubwa sana la walimu, kwani walimu takribari 270,000 wanahitajika ili kuweza kujaza uhitaji wa watoto wetu kuwa na walimu sahihi na kwa idadi sahihi ili waweze kufundishwa.”

“Kuajiri ni jambo moja na kuwa na uwezo wa kulipa mishahara kutokana na hali ya uchumi na uwezo wa nchi ni jambo jingine kitu kingine, wakati nchi inapojipanga kuweza kuajiri watu wengi lazima tuangalie watoto wetu katika hali ya sasa tunashughulika nao vipi, kwa hiyo ni mfumo ambao umekuja wakati sahihi.”

Mdee alisema kuwapo kwa mfumo huo ni suluhu ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kutokana na sasa kuwa dunia ni ya kidigitali na kuwa wao kama wabunge watasaidia katika kusukuma suala hilo ili serikali ilitekeleze nchi nzima.

“Natamani sana wakati majaribio yanaendelea, sisi kama wakilishi tulichukue na tulipeleke ili kuwe na fungu la kuhakikisha maeneo mengi katika shule za umma kunafunga madarasa janja,” alisema Mdee na kushauri pia Kamati ya Bunge ya Bajeti kuuoana mradi huu ili kuwe na msukumu wa kuutengea bajeti katika siku zijazo

Share To:

Post A Comment: