Wizara ya Madini iko mbioni kutekeleza Mkakati wa Mining for Better Tomorrow -BMT (Madini kwa kesho bora) utakao wawezesha vijana wa kitanzania kushirikishwa katika Sekta ya Madini ili kujiajiri pamoja na kuchangia katika mnyororo mzima wa shughuli za madini sambamba na mchango wa sekta katika Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla. 

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini,  Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 uliofanyika leo Januari 19, 2024 Mji wa Serikali Mtumba katika Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa mkakati huo umelenga kuwasaidia vijana pamoja na kuwashawishi ili waweze kushiriki uchumi wa madini kwa tija na kuwafanya kuwa wachangiaji wakubwa wa maendeleo kupitia Sekta ya Madini.

“Mkakati wa Mining for Better Tomorrow -BMT (Madini kwa kesho bora) utawawezesha vijana kwa kuwapatia ajira na kuwajengea uwezo, kuwapatia mitaji kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha, vifaa na mashine, kuwapatia wataalam waliopo katika sekta ili wapate ushauri elekezi katika utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na uthamini” amesema Dkt. Kiruswa.

Katika hatua nyingine,  Dkt.  Kiruswa amesema kuwa Wizara ya Madini  pia imeazimia kuendelea kuongeza taarifa za utafiti wa kina wa Madini.

“Lengo letu ni kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50 ya eneo la nchi nzima ifikapo mwaka 2030. Lengo likiwa ni kubaini maeneo yote yenye rasilimali madini na kuongeza wigo kwa Wachimbaji Wadogo, wa kati na Wakubwa, na kuwezesha kuendesha shughuli zao za uchimbaji bila kubahatisha na Serikali kuendelea kupata mapato ambayo yatawezesha kuimarisha sekta nyingine muhimu” ameongeza Dkt. Kiruswa. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa baraza hilo amesema kuwa ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakua na kuendelea kuwanufaisha watanzania ikiwa ni pamoja na kukuza mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa, katika Mwaka wa Fedha 2023/24 Wizara ilijiwekea vipaumbele ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuendeleza Madini Muhimu na Madini Mkakati, kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa Wachimbaji Wadogo, kuhamasisha shughuli za Uongezaji thamani madini, kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini na uanzishwaji wa Minada na Maonesho ya Madini ya Vito, pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Mheshimiwa Mgeni rasmi, napenda kutoa taarifa kuwa kumekuwa na utekelezaji mzuri wa malengo tuliyojiwekea katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2023 ambapo mafanikio mbalimbali yamefikiwa ikiwa ni pamoja na makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2023 yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 375.48 ikilinganishwa na shilingi bilioni 353.43 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23” amesema Mahimbali.  

Ameongeza kuwa, mafanikio mengine ni ongezeko la Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kwa robo ya Tatu ya Mwaka 2023 (Julai hadi Septemba 2023) hadi kufikia asilimia 10.2 ikilinganishwa na asilimia 9.6 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022, kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini ambapo katika kipindi cha robo ya Tatu (Julai hadi Septemba, 2023) ukuaji wa sekta ulifikia asilimia 10.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

“Mheshimiwa Mgeni rasmi, mafanikio mengine ni ununuzi wa mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uchimbaji kwa Wachimbaji Wadogo na utolewaji wa leseni 6,426 katika shughuli za madini kati ya leseni 4,614 zilizopangwa kutolewa katika kipindi husika” amesisitiza Mahimbali. 

Naye, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa amesema kuwa mafanikio mengi yamepatikana na yanaendelea katika Sekta ya Madini kutokana na Viongozi Wakuu kusimamia vema utekelezaji na kuhakikisha kuwa sekta inakua na kutoa mchango stahiki katika pato la taifa.

“Ndugu  Wajumbe, Mfano Mwaka 2017 wakati wizara inaanza mchango ulikuwa asilimia 4.2 na mwaka 2022 mchango ulifikia asilimia 9.1. Pia tunajua kuwa miradi mingi ya uchimbaji wa madini ya kinywe katika mikoa ya Lindi na Morogoro imesimamiwa vizuri na ifikapo 2025 tutakuwa na migodi mipya zaidi ya 3 itaanza kazi” amesema Ngulumwa. 

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, Wawakilishi wa Idara na Vitengo, Wawakilishi kutoka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini, Wawakilishi wa TUGHE kutoka Makao Makuu na ngazi ya Mkoa wa Dodoma, Afisa Kazi Mkoa wa Dodoma pamoja na Kamishna wa Kazi.

Share To:

Post A Comment: