Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemela amesema Mradi wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unasaidia kuongeza utoaji wa hati miliki za ardhi ya pamoja kwa wanandoa hatua inayopunguza nafasi ya kutokea kwa migogoro ya ardhi kwa wanandoa na familia zao.

Naibu Katibu Mkuu Kabyemela amesema hayo Februari 21, 2024 wakati anatambulisha kampeni ya “Kama Unampenda, Miliki Naye” wakati wa zoezi la Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Bunju A mkoa wa Dar es salaam.

“Tunafahamu kwamba watu kwenye familia baba na mama wanapendana, katika kipindi hiki cha mwezi wa wapendanao, ukimpenda mke au mume wako basi miliki naye ardhi ndiyo maana tunahamasisha kutoa hati za pamoja kwa mke na mume” amesema Naibu Katibu Mkuu Kabyemela.

Aidha, amewahimiza wanandoa kuepusha migogoro ya ardhi ambayo inaweza kutokea baadaye kwa kuonesha upendo baina yao inayokumba familia nzima ili umiliki wa ardhi hiyo ubaki kwa familia na watoto baada ya wazazi wao kufariki na waendelee kuwa katika mikono salama katika ardhi hiyo ambayo wataitumia kwa maendeleo yao bila matatizo yoyote.

Naibu Katibu Mkuu Kabyemela amesema Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi moja ya malengo yake ni kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi na takwimu zinaonesha wanawake wanaomiliki ardhi imeongezeka kutoka asilimia 25 na kufikia asilimia 41.

Naye Bi. Pamela Peter mkazi wa Wazo Hill Tegeta jijini Dar es salaam ameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuja na wazo la Kliniki hiyo ambayo imewarahisishia kupata hati kiurahisi na kwa muda mfupi.

Kwa upande wake Bw. Edimound Joseph mkazi wa Tabata mtaa wa Mfaume jijini Dar es salaam amesema Kliniki ya Ardhi imemsaidia kupata hati yake kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa hapo awali kitu ambacho hakuwahi kuwaza kupata hati hiyo kwa muda mfupi hatua inayomsaidia kuendelea na kazi nyingine za maendeleo ya familia yake na taifa.

Share To:

Post A Comment: