Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) leo tarehe 12 Machi 2024 ameweka jiwe la msingi jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Kampasi ya Dodoma katika eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.

Dkt. Mwigulu amesema jengo hilo litasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kubainisha matarajio ya serikali kwamba ujenzi wa miundombinu ya elimu unaoendelea IAA Kampasi ya Dodoma, Arusha, Babati na Kampasi tarajiwa ya Songea zitakuwa chachu katika kutoa elimu bora kwa Watanzania.

Aidha, Dkt. Mwigulu ameagiza uongozi wa IAA kuendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu hii, ili iweze kujengwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kuonesha thamani halisi ya fedha na kukamilika kwa wakati kwa ajili ya kutoa huduma stahiki.

Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa IAA kuendelea kubuni kozi zitakazowasaidia Watanzania kuelimika na kujikwamua kiuchumi na kufanya tafiti zitakazoleta tija katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa sita lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 4500 kwa wakati mmoja unatagharimu jumla ya shilingi bilioni 6.4 na litakapokamilika, IAA inatarajia kuanza kudahili wanafunzi wa shahada Dodoma katika mwaka wa masomo 2024/2025

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa kwa kutambua kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi, IAA kupitia Kampasi ya Dodoma itaendelea kutoa shahada ya uzamili kwa mwaka mmoja, kwa kufundisha vipindi vya darasani na mtandao kwa pamoja (blended) na kuanza kutoa masomo ya jioni kwa kozi za stashahada.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo IAA, Dkt. Mwamini Tulli ameishukuru Wizara ya Fedha kwa namna inavyounga mkono jitihada za chuo katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi unaendelea, huku akiahidi kuwa watasimamia fedha hizo vizuri na zitatimiza lengo lililokusudiwa.

 

 

 

 

 

 

Share To:

Post A Comment: