OR-TAMISEMI 


NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.  Deogratius Ndejembi amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Ndunguru kutuma timu ya wataalamu  kufanya uchunguzi kwenye ujenzi wa miradi ya shule za msingi zinazojengwa kupitia mradi wa BOOST na mradi wa jengo la Halmashauri ya Muheza mkoani Tanga.

Aidha amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dkt.Jumaa Mhina kumsimamisha kazi Mhandisi anayesimamia miradi hiyo ya BOOST kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wake na kusababisha kutokamilika kwa wakati.

Mhe. Ndejembi ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya BOOST, SEQUIP na jengo la Halmashauri kwenye Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Muheza ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi katika Mkoa wa Tanga.

“Namuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuleta timu ya uchunguzi kwenye shule hizi za BOOST kuja kuangalia bati, ubora wa bati, kuangalia pia ripoti ya Shirika la Viwango Nchini (TBS). Timu hii naiagiza ije hapa mara moja  ije ifanye uchunguzi huo na ikibainika kwamba bati hizi hazikidhi ubora basi mhandisi huyu wa BOOST achukuliwe hatua za kinidhamu pamoja na mhandisi wa halmashauri,”amesema.

Amesema timu hiyo ichunguze ujenzi wa jengo la halmashauri kwa kuwa hali yake hairidhishi na  hakuna kazi yoyote ya maana iliyofanyika licha ya kupelekewa fedha na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan toka Februari mwaka huu

“Baada ya uchunguzi huo tutachukua hatua stahiki kwa sababu hatuwezi kukubali kuona mtu yeyote anarudisha nyuma hatua kubwa za kimaendeleo zinazofanywa na Rais wetu  za kuwaletea watanzania maendeleo,” amesisitiza.

Share To:

Post A Comment: