Na John Walter-Manyara

Hadi kufikia sasa misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa na wadau mbalimbali wilaya ya Hanang'  mkoa wa Manyara palipotokea maafa ya maporomoko ya tope, mawe na magogo ina thamani ya shilingi bilioni  2,583,306,997.00 na fedha taslimu shilingi 5,208,729,711.00.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali  Mobhare Matinyi  katika taarifa yake ya desemba 24, 2023, Fedha taslimu zinajumuisha shilingi bilioni 2.5 zilizoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na shilingi 2,708,729,711.00 zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa inayosimamiwa na Ofisi ya  Waziri Mkuu. 

Kati ya fedha hizo, kiasi cha sh. 2,289,260,025.00 zimechangwa  na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kiasi kilichobaki cha sh. 419,469,152.00 kimechangwa na wahisani mbalimbali.

Serikali inaeendelea kuwashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao na kusisitiza  wanaoendelea kuleta misaada kujikita zaidi katika vifaa vya ujenzi.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Kambi  tatu zilizokuwa zinatoa huduma  zimefungwa baada ya waathiriwa  wote 690 kutoka kaya 140  kurejea makwao na kwa ndugu zao. 

Ikumbukwe kuwa Waathirika 534 walikuwa wakilala kambini  na 156 walikuwa wakija asubuhi na kuondoka jioni.

Utaratibu wa kugawa misaada hiyo unaoratibiwa na Idara ya Maafa chini ya Ofisi  ya Waziri Mkuu ikishirikiana na uongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya Hanang pamoja na kamati zao za usalama, unatumia watalaam kutoka Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. 

Kuhusu Mgawo wa misaada , taarifa imeeleza kuwa  unalenga kwanza waathirika 1,292 waliothibitika kupoteza nyumba zao ama kuharibika au kuingia tope. 

Idadi hii ilipatikana baada ya tathmini ya kina ya  picha za satelaiti, rekodi za sensa, ukaguzi halisi wa nyumba hadi nyumba na rekodi za serikali za mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na kata.

Utaratibu wa ugawaji misaada umewekwa kwa kubandika majina ya waathirika  kwenye ofisi za kata baada ya kukamilika kwa tathmini ambapo mhusika akifika  huelekezwa kituo chake cha kupokelea misaada.

Tangu wiki iliyopita wananchi  wamekuwa na ratiba za kwenda kupokea misaada kila siku kutokana na wingi wa  misaada hiyo. 

Kwa wastani kila kaya inapata chakula cha kutosha miezi sita au  zaidi ambapo kwa baadhi ya bidhaa kama sukari wananchi hao wanapewa ya  kutosha kutumia kwa zaidi ya miaka miwili kwa mujibu wa vipimo vya lishe.

Misaada inayotolewa ni chakula cha mahindi, ngano, mchele, unga wa mahindi,  unga wa ngano, maharage, mafuta ya kula, maziwa, unga wa lishe kwa watoto,  mayai, sabuni, magodoro, mablanketi, mashuka, mikeka, ndoo, majiko ya kupikia  ya gesi na mitungi yake, masufuria, nguo, viatu, kandambili na vingine vingi.

Idadi ya watu waliopoteza maisha imebakia kuwa 89 tangu tarehe 11 Desemba na mwili mmoja wa mtoto wa kike bado haujatambuliwa. 

Maafa haya yalitokea  alfajiri ya tarehe 3 Desemba, 2023, baada ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang kuvamia vijiji vinne vilivyokuwa kando  ya mlima Hanang na kata nne za mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang.

Hadi sasa majeruhi wanne bado wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo mjini Babati na mmoja amepelekwa Hospitali ya  Benjamin Mkapa jijini Dodoma. 

Serikali imegharamia matibabu, mazishi na  kutoa mkono wa pole kwa wafiwa. Majeruhi wote walifikia jumla ya 139.

Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa akaunti ya kielektronikia kuchangia fedha za misaada  yenye nambari 9921159801 iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na inayopokea fedha  kupitia benki yoyote nchini na pia kutoka nje ya nchi kwa kutumia swift code ya  TANZTZTX. Miamala yote inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG. 


Share To:

Post A Comment: