Na Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema kuwa litawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto wanatumia kigezo cha mwisho wa mwaka kuingiza vyombo vyao ambavyo vinachangamoto za kiufundi na kutumia kigezo cha mwisho wa mwaka kusafirisha abiria maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa mapema leo Disemba 03,2023 na Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi Jirani huku akibanisha kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wamiliki kutumia kigezo cha wingi wa abiria na mwisho wa mwaka kuingiza magari mabovu barabarani.

SSP Zauda ameongeza kuwa Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama Barabarani Mkoani humo hakitowafumbia macho wamiliki watakao bainika kuingiza magari mabovu barabarani huku  akisema kikosi hicho kitaendelea kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto mara kwa mara na kutoa elimu kwa madereva na abiria wanaotumia vyombo hivyo.

Aidha amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kumaliza kabisa ajali ambazo zimekuwa zikisababisha ulemavu na kuwaacha wananchi wakiwa na ulemavu wakudumu ambapo amewataka madereva ambao wamekuwa wakiendesha umbali mfupi kuwatumia madereva wazoefu kuwaendesha kama wanakwenda safari ndefu.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa wazazi wanatumia kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kuwasafirisha watoto wadogo Kwenda kuwasalimia ndugu na jamaa maeneo tofauti tofauti  kuhakikisha watoto hao wanakuwa na uangalizi wa karibu ili kupunguza vitendo vya kupotea kwa Watoto kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Kwa upande wake Mchungaji Getruda Kyando ambaye anatumia usafiri wa mabasi yanayokwenda maeneo tofauti tofauti hapa nchini Pamoja na kuwaomba Jeshi hilo kufanya kaguzi za mara kwa mara amekipongeza kikosi hicho kwa kutoa elimu na mawasiliano ya moja kwa moja kwa abiria ambayo yatasaidia kutoa taarifa kwa wakati pindi  madereva wanapokiuka sheria za usalama Barabarani.

Nao baadhi ya madereva wanaofanya safari zao ndani na nje ya nchi wamesema kumekuwepo na ongezeko la magari kipindi hiki cha mwisho wa mwaka huku wakiwataka madereva wenzao wasiofuata sheria za usalama barabarani kuhakikisha wanafuta sheria hizo ili kupunguza ajali .
Share To:

Post A Comment: