Na John Walter-Babati

Wananchi wa kijiji cha Maweni kata ya Qash wamemshukuiru Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo kwa kuwasaidia kuchimba Mtaro utakaosaidia kufikisha maji kijijini hapo.

Wananchi hao wamemwambia Mbunge huyo kuwa ni muda mrefu wameteseka kupata huduma ya maji safi na salama na kwamba kwa sasa wanatumia maji ambayo sio salama kwa afya zao kwani  yamesababisha wengine kupinda miguu kijiji cha Endadosh.

Mkazi wa kijiji cha Maweni Asha Paulo amesema Sillo kwa msaada huo amewatua ndoo kichwani kina mama na watafanya sherehe kubwa kijijini hapo na kumualika mbunge huyo kwa furaha waliyonayo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Maweni Amos Gara amesema kupitia vikao walikubaliana kuanza kuchimba mtaro kwa nguvu zao ila walikwama kutokana na mawe mengi ardhini.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) Mhandisi Sebastian  Honolath amesema wataanza kuweka mabomba baada ya mtaro kukamilika.

Wazee wa Maweni wamemuombea dua mbunge huyo wakimwaahidi kusheherekea naye pindi maji hayo yatakapofika kijijini hapo kwani hwakuwahi kuwa na maji tangu nchi ipate uhuru.

"Tuliwahi kula mbuzi na Mbunge wetu, na siku tunakunywa maji safi, tutakula ng'ombe hapa" alisema Mzee Bura Haraja

Akizungumza na wananchi hao, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo amesema ameamua kuwatua ndoo kichwani kina mama na kuwapunguzia mzigo kina baba kutoa fedha za maji kwa kulipa gharama za mtambo wa kuchimba mtaro.

Katika kijiji hicho wananchi hulazimika kununua maji kwa shilingi 700 kwa ndoo na wakati huo wana mifugo.

Share To:

Post A Comment: